Zenj FM

Jaji Kazi: Waangalizi wazingatie uadilifu na mipaka ya mamlaka yao

27 October 2025, 9:02 pm

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jaji Gorge Joseph Kazi .

Na Mary Julius.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jaji Gorge Joseph Kazi  amewataka waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uangalifu, uhuru na uadilifu kwa kuzingatia malengo ya kazi zao, huku wakiheshimu sheria za Zanzibar na za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwenyekiti ametoa wito huo katika mkutano maalum kati ya Tume na taasisi za waangalizi wa uchaguzi, uliofanyika kwa lengo la kuwapa maelekezo kuhusu utaratibu wa uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti amesema waangalizi wana wajibu wa kufuata mipaka ya mamlaka yao kwa kuhakikisha hawaingilii kazi za wasimamizi wa uchaguzi, wagombea, au wapiga kura.

Aidha, amewakumbusha kutunza siri za upigaji kura na kuwasilisha kwa Tume nakala za taarifa na maelezo wanayokusanya wakati wa zoezi la uangalizi.

Ameongeza kuwa ripoti zinazowasilishwa na makundi ya waangalizi zimekuwa na mchango mkubwa katika kubaini mianya na changamoto zinazojitokeza wakati wa uchaguzi, jambo linalosaidia Tume kufanya maboresho ya sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili kuongeza ufanisi katika chaguzi zijazo.

Sauti ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jaji Gorge Joseph Kazi .