Zenj FM

Polisi watia neno kwa wanaopanga kuvuruga uchaguzi

23 October 2025, 8:01 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah.

Na Mary Julius.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limesema limejipanga kikamilifu kuimarisha doria na usalama katika maeneo yote ya mkoa huo siku ya kupiga kura ya tarehe 29 Oktoba, ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu la kitaifa.

Akizungumza katika kipindi cha Mwangaza wa Habari kinachorushwa na Zenji FM, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah amesema uchaguzi bila vurugu inawezekana, na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuiweka rekodi mpya ya uchaguzi wa amani Zanzibar.

akizungumzia taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu maandamano, Kamanda Shillah amesema Jeshi linafuatilia kwa karibu minong’ono hiyo, na limejipanga kuwachukulia hatua wote watakaopanga kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume cha sheria.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah

Akitolea ufafanuzi wa kura ya mapema, ambapo baadhi ya viongozi wanadaiwa kuwataka wanachama wao kuwasindikiza wapiga kura.

Kamanda amesema Zoezi la uchaguzi ni la kisheria na  Kama kungekuwa na haja ya kusindikiza watu kupiga kura Oktoba 28, sheria ingesema hivyo  Wale wasiopaswa kupiga kura siku hiyo amewataka kubaki nyumbani na kusubiri tarehe 29.

Aidha Kamanda Shillah ametoa wito kwa wananchi wa Kusini Unguja kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kutii miongozo ya uchaguzi na vyombo vya usalama, ili kuendelea kuilinda amani ya Zanzibar.