Zenj FM

Wanaharakati wataka serikali iridhie itifaki ya haki za watu wenye ulemavu Afrika

23 October 2025, 12:27 pm

Mshiriki wa mafunzo hayo akichangia mada .

Na Ivan Mapunda.

Wanaharakati na wadau wa watu  wenye ulemavu nchini wameiomba Serikali kuridhia itifaki ya masuala ya watu wenye ulemavu Afrika ili kuondokana na vitendo vya ubaguzi na kunyimwa haki zao za kibinadamu.

Hayo yameelezwa Unguja , Afisa Sheria Mkuu wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Afisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar Idissa Khamis Daima wakati akizungumza kwenye mafunzo ya waandishi wa habari yaliyondaliwa na WUKU  kuhusu faida za itifaki hiyo na namna inavyolinda haki za watu wenye ulemavu.

Itifaki hiyo inatokana na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu uliopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika katika Mkutano wa 30 wa kawaida wa Bunge mnamo Januari 2018 na hadi sasa Tanzania bado haijaridhia.

Akizungumza kuhusu faida za itifaki hiyo, afisa Daima , amesema katika mkataba huo kuna haki za watu wenye ulemavu katika masuala ya elimu, ajira, afya, fursa za kiuchumi na miundombinu inayofikika.

Pia, amesema mkataba huo unaongelea masuala ya uwakilishi wa watu wenye ulemavu katika shughuli za kisiasa na umma, haki za wanawake, wasichana na watoto.

Aidha amesema  ni muhimu kwa Tanzania kuridhia mkataba huo ambao unakwenda kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu kwa Afrika zinalindwa kwa kuwa kuna mambo hayafanani na nchi zingine zilizoendelea.

Sauti ya Afisa Sheria Mkuu wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Afisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar Idissa Khamis Daima.

Naye Mratibu wa Mradi wa Wanawake Wenye Ulemavu Kusini Unguja WUKU Khayrun Khalid Mambo , amesema  WUKU inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kutoa hamasa kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa na mkataba huo kuridhiwa.

Aidha Amesema hadi sasa nchi 16 zimeridhia na kwa kupitia vyombo vya habari wananchi watajua umuhimu wa mkataba huo kwa Tanzania na kuhamasisha serikali kuridhia mkataba huo.

Sauti ya Mratibu wa Mradi wa Wanawake Wenye Ulemavu Kusini Unguja WUKU Khayrun Khalid Mambo ,

Naye, Muwezeshaji katika mafunzo hayo Mary JuliUs Kitipwi  amesema wanawake wenye ulemavu wanaomba serikali iridhie mkataba huo ili kuweka uchechemuzi wa haki zao za kiafya kwenye sera na sheria zinazotungwa.

Sauti ya Muwezeshaji katika mafunzo hayo Mary JuliUs Kitipwi .