Zenj FM

Makundi maalum yaahidiwa mazingira rafiki kwenye uchaguzi mkuu wa 2025

22 October 2025, 9:27 pm

Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Idrissa Haji Jecha akizungumza wakati wa akifungua mafunzo kwa wadau wa makundi maalum yaliyofanyika katika ukumbi wa ZEC uliopo Maisara.

Mary Julius.

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema itahakikisha makundi yote ya watu wenye mahitaji maalum yanashiriki  katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 bila kubaguliwa.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo kwa wadau wa makundi maalum yaliyofanyika katika ukumbi wa ZEC uliopo Maisara, Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Idrissa Haji Jecha amesema Tume imejiandaa kuhakikisha haki ya kila raia ya kupiga kura inalindwa na kutekelezwa kwa usawa.

Amesema Tume hiyo inatambua umuhimu wa watu wenye ulemavu, wazee na makundi mengine maalum katika mchakato wa kidemokrasia, hivyo imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.

Jecha amesema maandalizi hayo yanahusisha kuweka mazingira rafiki na miundombinu maalum katika vituo vya kupigia kura, ikiwemo maandishi ya nukta nundu kwa wasioona na huduma za wakalimani kwa wenye ulemavu wa kusikia.

Aidha Ametoa wito kwa jamii kushirikiana na Tume hiyo kwa kutoa taarifa za watu wenye mahitaji maalum katika maeneo yao ili kuwezesha maandalizi bora kabla ya siku ya kupiga kura.

Sauti ya Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Idrissa Haji Jecha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Wapiga Kura na Mawasiliano kwa Umma, Juma Sanifu Juma akiwasilisha mada kuhusu nafasi ya makundi maalum katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, amesema  ZEC inatekeleza sera ya kuyapa kipaumbele makundi hayo.

Sauti ya Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Wapiga Kura na Mawasiliano kwa Umma, Juma Sanifu Juma.
Mshiriki Machano Chum Haji akiwa katika mafunzo ya Matumizi ya Kisaidizi cha kupiga kura kwa watu wasioona.

Katika mafunzo hayo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetoa elimu maalum ya namna ya kutumia karatasi za kupigia kura kwa mfumo wa kugusa na kutambua kwa vidole, maarufu kama Nukta Nundu (Tactile).

Akizungumza katika mafunzo hayo Afisa Elimu kwa Mpiga Kura Ali Ramadhani Ali amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha watu wenye ulemavu wa kuona wanatumia haki yao ya kikatiba kwa uhuru na bila utegemezi kwa wengine.

Sauti ya Afisa Elimu kwa Mpiga Kura Ali Ramadhani Ali.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa hatua hiyo muhimu, wakisema imeonyesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha kila raia, bila kujali hali yake, anashiriki ipasavyo katika Uchaguzi Mkuu.

Sauti za washiriki wa mafunzo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na ZEC, jumla ya watu 7,891 wenye ulemavu wamejiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa mwaka huu, hatua inayotajwa kuwa ni mafanikio makubwa ya juhudi za tume hiyo katika kujumuisha makundi yote ya kijamii.