Zenj FM

Polisi: Hatutakubali uvunjifu wa amani siku ya kupiga kura

21 October 2025, 9:28 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Mchomvu.

Na Mary Julius.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Mchomvu amesema Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama wa hali ya juu.

Kamanda Richard ameyasema hayo katika kipindi cha Mwangaza wa Habari kinachorushwa na Zenj Fm , Kamanda  amesema hali ya utulivu iliyopo sasa inaleta heshima kubwa kwa nchi na ni jukumu la kila mwananchi kuilinda.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha kuwa wananchi wanatekeleza haki yao ya kupiga kura bila hofu.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Mchomvu.

Kuhusu kauli za baadhi ya wagombea na wafuasi wao wanaotaka “kulinda kura,” Kamanda amefafanua kuwa jukumu hilo ni la Jeshi la Polisi, ambalo tayari limejipanga kulinda kura hizo kwa weledi na uadilifu.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Mchomvu.

Aidha, Kamanda ametoa onyo kali kwa watu wote wanaopanga kufanya vitendo vya uhalifu siku ya kupiga kura, akisema Jeshi la Polisi limejipanga na lina vifaa vipya vya kudhibiti uhalifu na litachukua hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Amehitimisha kwa kuwataka wanasiasa kufuata ratiba ya kampeni iliyopangwa kisheria, na wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo hadi siku ya kupiga kura na baada ya kupiga kura.