Zenj FM
Zenj FM
19 October 2025, 9:18 pm

Na Mary Julius.
Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Awadhi Ali Saidi, ameliomba Jeshi la Polisi kuendeleza mashirikiano mazuri yaliyopo na kuendelea kujitolea kwa hali ya juu katika kulinda usalama na utulivu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa October 29, kwa maslahi ya Taifa.
Akifungua mafunzo maalum kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi wa Wilaya zote za Unguja katika ukumbi wa Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid uliopo Makao Makuu ya ZEC Maisara, Wilaya ya Mjini Unguja,kuhusu majukumu yao wakati wa uchaguzi, Awadhi amesema usalama, utulivu na haki katika uchaguzi vinategemea kwa kiasi kikubwa busara, uadilifu na weledi wa Jeshi la Polisi katika kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha uchaguzi, mazingira huwa na hisia kali na mikusanyiko mingi, hivyo ni wajibu wa Jeshi la Polisi kulinda usalama wa watu wote bila ubaguzi.
Aidha, amewataka maafisa wa Polisi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uweledi, uadilifu na bila upendeleo, hasa katika kipindi cha kura za mapema na siku ya uchaguzi.
Akitoa mada ya kwanza Katika mafunzo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Jaala Makame, amesisitiza umuhimu wa Polisi kuelewa wajibu wao katika kusimamia mazingira salama na tulivu wakati wa uchaguzi.
Naye Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mwanamkuu Gharib Mohammed, akiwasilisha mada kuhusu ulinzi wakati wa maandalizi ya uchaguzi, ameeleza kuwa Jeshi la Polisi linapaswa kuhakikisha Wapiga kura wenye mahitaji maalum wanapewa kipaumbele vituoni, pamoja na kuhakikisha Wapiga kura wanaondoka mara baada ya kupiga kura.
Wakichangia katika mafunzo hayo, baadhi ya maafisa wa Polisi wameiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar kutoa mafunzo kama hayo kwa vikosi vingine vya ulinzi na usalama vya SMZ, pamoja na usafiri kuwapatia usafiri maafisa wa Polisi wakati na baada ya uchaguzi.
Akifunga mafunzo hayo, Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Juma Haji Ussi, amesema ZEC imejipanga kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na unaozingatia misingi ya kidemokrasia, na kwamba mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila mchango mkubwa wa Jeshi la Polisi.
Ameongeza kuwa maafisa wa polisi waliopata mafunzo hayo wanapaswa kuwafikishia wenzao elimu hiyo ili kuhakikisha mwongozo wa uchaguzi unazingatiwa kwa wote.