Zenj FM
Zenj FM
19 October 2025, 1:10 am

Na Ivan Mapunda.
Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Mfenesini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Asha Juma Kombo, amesema endapo atapata ridhaa ya wananchi kuwa Mbunge wa jimbo hilo, atahakikisha anatoa mikopo isiyo na riba kwa wajane na wajasiriamali wadogo ili kuwawezesha kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Mkoa wa Magharibi Mjini, Asha amesema Ilani ya CCM imeweka mkazo mkubwa kwa makundi maalum, ikiwemo wajane na wajasiriamali, kwa lengo la kuboresha maisha yao kupitia mifumo ya mikopo nafuu na isiyo na riba.
Asha aliongeza kuwa, akichaguliwa, atashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha waendesha bodaboda wanapatiwa maeneo rasmi na rafiki ya kufanyia kazi zao kwa usalama na ufanisi zaidi, ili kuendeleza juhudi za kujiajiri.
Kwa upande wake, Mgombea Uwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman Saidi, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, jimbo hilo limepata maendeleo makubwa katika sekta za miundombinu, maji, afya na elimu, hivyo kuwaomba wananchi kuendelea kuwaamini viongozi wa CCM ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Baadhi ya wananchi walioshiriki mkutano huo waliwataka wagombea hao, endapo watapata ridhaa ya wananchi, kuhakikisha wanatekeleza ahadi zao za kutoa mikopo nafuu itakayosaidia kupunguza changamoto za kiuchumi katika jamii.