Zenj FM

Mchango wa wanaume  ni chachu ya ushindi kwa wanawake 2025

16 October 2025, 2:49 pm

Baadhi ya wananchi.

Na Ivan Mapunda.

Zanzibar ya sasa inashuhudia mabadiliko makubwa katika ushiriki wa wanawake katika uongozi, ikilinganishwa na enzi za zamani.

Kwa mara ya kwanza tangu Mapinduzi ya 1964, wanawake wanashikilia nafasi muhimu, ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Kulingana na Sera ya Jinsia ya Tanzania (2000-2020), ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya kisiasa ulikuwa chini, lakini hadi kufikia mwaka 2020, idadi iliongezeka na kufikia asilimia 36 kutokana na juhudi za mashirika binafsi, Serikali na wanaharakati.

Katika uchaguzi mkuu wa 2020, wanawake wapatao 300 walijitokeza kuwania nafasi za uongozi kupitia vyama mbalimbali kama CCM, CHADEMA, ACT Wazalendo, na NCCR Mageuzi.

Hata hivyo, idadi ya wanawake walioteuliwa ilikuwa chini, ingawa kulikuwa na ongezeko kubwa la wanawake waliojitokeza ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.

Ni kweli kuwa bado changamoto kubwa katika Jamii inayotuzunguka kukubali nafasi za Wanawake katika kuongoza licha ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaongozwa na Mwanamke kwa mafanikio.

MAONI YA WANAUME

Suleiman Ali Seifa  37, mkaazi wa Unguja Ukuu  ambae ni mwanachama wa chama Act Wazalendo anasema kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa wanawake kushiriki kuwania nafasi za uongozi ili kuwa sauti ya wanawake wengine na kuleta mabadiliko ya kijamii na kisiaasa.

Ukweli kuwa ni wakati wa Mapambano ili kuhakiksha usawa wa kijinsia ufikiwa Zanzibar na Wanawake wanashika nafasi za uongozi bila kuhusisha rushwa na kuvunja utaratibu badala yake tuwajengewe uwezo ili kusaidia wanawake wengine na jamiii kwa ujumla,” amesema.Mimi nipo tayari kuchagua Kiongozi mwanamke ambae atapitishwa na chama chetu kutokana kuwa Wanawake wanapoongoza kwa wingi wanaweza kusaidia kuondoa vikwazo vya kijinsia na kuhimiza usawa katika jamii lakini pia wanaweza kuwa chachu ya hamasa kwa vijana na wasichana, kuonyesha kuwa wanaweza kufikia malengo makubwa,” amesema.
Ibrahim  Salum Said  28, mkaazi wa mtoni unguja unguja anasema kuwa, wanawake anaweza kuleta mtazamo tofauti katika uongozi kwa kusaidia kukuza uchumi wa jamii na hata mtu mmoja mmoja.

“Viongozi wanawake wengi wao huwa ni waadilifu si rahisi kusikia ni mafisadi hivyo tukiwa na viongozi wanawake tunaweza kupiga hatua zaidi za kukula uchumi wa jamii na hata mtu mmoja mmoja,” ameeleza.

Hata hivyo amesema kuwa, wanawake viongozi mara nyingi huleta mtindo wa uongozi wa ushirikiano, unaoweza kusaidikatika kujenga jamii zenye umoja na mshikamano.

Said Omar Mohamed  47, mkaazi wa Fuoni Jitimai  anasema kuwa, wanapaswa kuchaguliwa kwa wingi kutokana kuwa wanawake wana sifaa za kipekee tofauti na wanaume.

“Sifa ya wanawake ni ya kipekee tofauti na wanaume ni vigumu sana kuina kiongozi wa kike mbadhirifu wa mali za umma, wanawake wana huruma kuliko wanaume, wanawake ni wanunifu katika kuingoza,” ameeleza.

SHERIA INASEMAJE

Ali Almasi Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii Zanzibar anasema kuwa kutokana na misingi ya usawa na haki za binadamu wanawake wanapaswa kuwa viongozi katika jamii zinazotuzunguka.

“Hii ina maana kwamba kila mtu anayo fursa ya kuwa sehemu uongozi katika nchi yetu kama ambavyo ibara 21(1) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katiba ya Zanzibar ibara sawa na hiyo,”.

Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina anasema kuwa, sheria namba No.5 ya Mwaka 1992, sura ya 258 inaweka masharti kwa vyama vya siasa nchini kuhakikisha usawa wa Kijinsia katika kuandaa na kutekeleza sera.

“Licha ya Sheria kuweka masharti lakini bado kuna changamoto patika utekelezaji wake kwa baadhi ya vyama via siasa linapokuja suala la kuwapoa nafasi wanawake,” amesema Thabit Idarous Faina.

KAULI ZA WANAHARAKATI

Salma Omary Zeeyn  Wakili wa  Jumuiya Ya Wanawake ZAFELA mkaazi wa shehia ya Nyerere  anasema jamii bado haina uelewa juu ya umuhimu wa wanawake kuwa viongozi wa kisiasa jambo linalopelekea kuzaliwa kwa changamoto nyingi.

“Hatuna budi kuongeza juhudi katika kutoa elimu kuhusu wanawake na uongozi ili kufikia usawa wa kijinsia ukizingatia tunaelekea katika uchaguzi mkuu,” anasema.

Katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia Makini Ameir Hassan Ameir anasema kwamba chama chao kwa sasa kimeweka utaratibu mzuri wa wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi licjha ya wanawake kukabiliwa na changamoto mbalimbali.

Rajab Mbarouk Mohamed Mkuu Wa Itifaki Taifa Chama Chama Cha wananchi CUF  anasema kuwa kuna kila haja ya jamii na hata wadau wa vyama vya siasa kuungana pamaoja kuhamasisha umuhimu wa nafasi za uongozi.

HITIMISHO
Kuna hitajika juhudi za pamoja za kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia na kutoa elimu juu ya faida za Wanawake kuwa viongozi.

Pia, kuunga mkono sera zinazowasaidia wanawake na kujenga mifano chanya ya uongozi wa wanawake ni muhimu ili kubadilisha mitazamo ya kijamii.

Kufanya maboresho ya miongozo iliyopo ili kuleta usawa wa kijinsia.