Zenj FM
Zenj FM
9 October 2025, 12:08 am

Na Mary Julius
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa kupitia Chama cha Demokrasia MAKINI Ameir Hassan Ameir, ameahidi kupunguza gharama za maisha kwa wananchi wa Zanzibar kwa kupunguza bei ya vyakula na huduma muhimu, endapo chama chake kitapewa ridhaa ya kuunda serikali.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Daraja Bovu Madukani, Wilaya ya Magharibi “A”, Ameir amesema serikali ya Demokrasia Makini itapunguza bei ya mchele wa basmati hadi shilingi 1,000 kwa kilonakufuta ushuru kwa wafanyabiashara wanaoingiza vyakula muhimu nchini, ili kuhakikisha kila Mzanzibari anapata chakula bora kwa bei nafuu.
Kwa upande wa elimu Ameir amesema chama chake kitahakikisha elimu inatolewa bure kuanzia ngazi ya chekechea hadi chuo kikuu, sambamba na kuanzisha bodi maalum ya elimu ya juu itakayowasaidia wanafunzi kupata ufadhili wa masomo bila usumbufu.
Mgombea huyo amesema wanawake watawezeshwa kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba ya shilingi milioni kumi (10,000,000) kwa kila kikundi, ili waweze kujitegemea na kuendesha biashara zao kwa uhuru.
Aidha, Amesema vijana watanufaika na mradi wa pikipiki (boda boda) 100,000 ambazo watapewa bila malipo ili kujiongezea kipato na kupunguza tatizo la ajira.

Kwa upande wake, Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia chama chama Demokrasia MAKINI Azza Suleman Haji amesema chama chake kina vipaumbele vitatu vikuu Elimu, Afya na Kilimo ambavyo vitakuwa msingi wa ustawi wa wananchi.
Amesema serikali yake itahakikisha Zanzibar inajitosheleza kwa chakula kupitia kilimo cha kisasa, ugawaji wa mbegu bora na pembejeo bure kwa wakulima.
Aidha, Mgombea Mwenza amewataka vijana kote nchini kuendelea kudumisha amani kwa kufuata miongozo na sheria zilizowekwa na Serikali, hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu. Amesisitiza kuwa bila amani, ahadi zote zinazotolewa na wagombea haziwezi kutekelezwa ipasavyo.