Zenj FM

Vyama vya siasa vyahimizwa kuandaa mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu katika kampeni

7 October 2025, 4:02 pm

Afisa Programme wa Masuala ya Kuhamasisha Wanawake katika uongozi kutoka TAMWA ZNZ  Khairat Haji .

Na Berema Suleiman Nassor.

Vyama vya siasa vyahimizwa kuzingatia ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye mikutano ya kampeni.

 Akizungumza  kwa niaba ya taasisi zinazoshughulikia masuala ya uongozi wa wanawake Afisa Programme wa Masuala ya Kuhamasisha Wanawake katika uongozi kutoka TAMWA ZNZ  Khairat Haji amesema   vyama vya siasa  viweze kuzingatia na kuhakikisha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika mikutano ya kampeni zinazoendelea ili kuweza kufatilia sera mbalimbali zinazotolewa na wagombea.

Sauti ya Afisa Programme wa Masuala ya Kuhamasisha Wanawake katika uongozi kutoka TAMWA ZNZ  Khairat Haji

Katika taarifa ya pamoja taasisi hizo zimeeleza kuwa kuna baadhi ya vyama vimeshuhudiwa vikiendesha mikutano ya kampeni bila ya kuandaa mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu hali inayopelekea kushindwa kushiriki na kufuatilia kampeni zinazoendelea kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

 Taarifa hiyo imesema kwa mfano ni chama kimoja tu ambacho kimeweka wakalimani katika mikutano yake na ambao huonekana zaidi wakati wa mikutano inayofanywa na mgombea wa Uraisi na hivyo katika nafasi nyengine mazingira hayo bado yanakosekana isipokuwa kwa jimbo moja tu katika mkoa wa mjini magharibi ambapo kumeandaliwa wakalimali maalum kwa ajili ya kundi hilo muhimu.

Taasisi hizi zinasisitiza vyama kuiga mfano huo wa wakalimani na kuhakikisha maeneo ya mikutano yanafikika kwa urahisi, kuweka maandiko makubwa na vifaa vya msaada wa kusikia katika maeneo yote katika mikutano yote ya wagombea wa Uraisi na nafasi nyengine zikiwemo za Uwakilishi, Ubunge na Udiwani ili suala la ushiriki na ushirikishwaji liwe na maana zaidi na kujenga demokrasia ya kweli.

Amesema  Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) jumla ya watu wenye ulemavu wapatao 8,021 wanatarajiwa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 visiwani Zanzibar.

Sauti ya Afisa Programme wa Masuala ya Kuhamasisha Wanawake katika uongozi kutoka TAMWA ZNZ  Khairat Haji .

Sheria ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Namba 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 29 kinaeleza umuhimu wa watu wenye ulemavu kuweza kufikia miundo mbinu mbali mbali pamoja, taarifa, mawasiliano na haki zote za kibinaadamu na za msingi.

 Kutokana na haki walizopewa watu wenye ulemavu za kushiriki kikamilifu katika kampeni za kisiasa, viongozi wa vyama vya siasa wanawajibika kuhakikisha ushiriki huo unatekelezwa bila vikwazo kwa kuweka miundombinu rafiki katika viwanja vya kampeni, kutoa taarifa zinazoweza kufikiwa kwa urahisi, na kuwezesha upatikanaji wa usafiri pamoja na vifaa vya msaada.

Aidha, Tume ya Uchaguzi na wadau wengine wanapaswa kutoa motisha kwa vyama na wagombea wanaojumuisha watu wenye ulemavu, hatua ambayo itachochea usawa na kudhihirisha mfano bora demokrasia iliyo sawa.  

Taasisi hizo ambazo ni pamoja na Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Zanzibar Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake (ZAFELA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) zimesema kuwa kuna baadhi ya vyama havijazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu katika mikutano yao jambo ambalo linawanyima haki yao ya msingi ya kufuatilia sera za vyama na hivyo kufanya maamuzi sahihi ya kura zao.