Zenj FM
Zenj FM
1 October 2025, 10:27 pm

Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba ya wageni (villa) na kusababisha hasara kubwa ya mali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah, amesema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 30 Septemba 2025, majira ya saa 9:15 alasiri, katika Mbuyuni Beach Villa, iliyopo Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Paskalina Marro Bhoke (22), Mkabila wa mkurya, mkazi wa Jambiani na Pili Haule Medard (25), Mngoni, mkazi wa Jambiani.
Inadaiwa kuwa kwa pamoja walichoma moto Villa namba 3 ya hoteli hiyo, na kusababisha kuungua kwa paa la jengo pamoja na samani zilizokuwemo ndani ,thamani ya mali zilizoteketea inakadiriwa kufikia Shilingi Milioni 20.
Akizungumzia chanzo cha tukio, Kamanda Shillah amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa tukio hilo linahusishwa na mgogoro wa kimapenzi kati ya mtuhumiwa Paskalina na Alexander Gyamaty, raia wa Ujerumani, ambaye alikuwa amefikia kwenye villa hiyo kama mgeni.
Katika tukio hilo, hakuna madhara ya kibinadamu yaliyoripotiwa na watuhumiwa wote wawili wamekamatwa na mahojiano yanaendelea ili kukamilisha uchunguzi.
Aidha Kamanda Shillah ametoa wito kwa wamiliki wa nyumba za wageni kuhakikisha kuwa Wageni wote wanaoingia wanatambuliwa na kusajiliwa kikamilifu katika rejista na wanatambua pia watu wanaoambatana na wageni hao, kwa lengo la kuimarisha usalama na kuepusha matukio ya uhalifu.