Zenj FM
Zenj FM
25 September 2025, 7:47 pm

Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa njia ya amani, na kuwahakikishia kuwa ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ili kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na salama.
Na Mary Julius.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Mchomvu, amesema Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa hali ya usalama na utulivu inadumishwa katika kipindi chote cha kampeni hadi kufikia uchaguzi mkuu.
Akizungumza katika kipindi cha Mwangaza wa Habari kinachorushwa na Zenji FM Radio, Kamanda Mchomvu amesema vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimeweka mikakati madhubuti kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, utulivu na kwa kuzingatia misingi ya haki na sheria.
Aidha, Kamanda ametoa wito kwa madereva wa magari kuzingatia matumizi sahihi ya leseni zao kwa kubeba mizigo au abiria kulingana na aina ya leseni waliyonayo.
Amesisitiza kuwa ni marufuku kwa magari ya mizigo kubeba abiria, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za usalama barabarani.
Amewataka madereva kuacha tabia ya kufunika namba za usajili wa magari kwa kuweka matangazo ya wagombea wa kisiasa, na badala yake wazingatie sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.
Kuhusu uwepo wa watoto katika mikutano ya kampeni, Kamanda Mchomvu ametoa rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wanabaki nyumbani na kushiriki katika shughuli zinazowahusu, kwani hawaruhusiwi kushiriki katika mchakato wa upigaji kura.