Zenj FM
Zenj FM
25 September 2025, 7:21 pm

Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limewataka wananchi kuwa na uelewa wa vigezo vya kisheria vinavyohitajika ili kesi za udhalilishaji ziweze kufikishwa mahakamani na haki kutendeka kwa waathirika.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Zenji FM, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Mkoa huo, Kamanda Vicent Innocent, amesema ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na vyombo vya dola ni muhimu katika kufanikisha upelelezi na mchakato wa kisheria wa kesi hizo.
Kamanda Vicent amebainisha kuwa ongezeko la matukio ya udhalilishaji kuripotiwa katika Wilaya ya Kati ni ishara ya mafanikio ya juhudi za Jeshi la Polisi katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu udhalilishaji na namna ya kuripoti matukio hayo.
Amesema kuwa mwamko huu unaonesha jamii imeanza kuelewa umuhimu wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Sadiki Ali Sultan, amesema mchakato wa kufikisha kesi ya udhalilishaji mahakamani unahusisha hatua kadhaa za kisheria, ikiwemo Kuwasilisha taarifa rasmi kwa Jeshi la Polisi, Kufanyika kwa upelelezi wa kina,Kuwasilisha jalada kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), na haimaye, kufikishwa kwa kesi mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa.
Inspekta Sadiki pia ametaja changamoto kubwa kuwa ni ukosefu wa uelewa wa kisheria miongoni mwa wananchi, hali inayosababisha baadhi yao kusitisha kesi katika ngazi ya polisi bila kuendeleza mchakato wa kisheria, jambo linalokwamisha juhudi za haki.
Aidha Jeshi la Polisi linatoa wito kwa jamii kuacha kufuata mitazamo binafsi na badala yake kufuata taratibu za kisheria, ili kuhakikisha waathirika wa vitendo vya udhalilishaji wanapata haki stahiki.