Zenj FM

CCM yaweka mikakati madhubuti ya kuongeza ajira kwa vijana

19 September 2025, 6:28 pm

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Na Mary Julius.

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ukuaji wa uchumi ni matokeo ya utekelezaji mzuri wa sera ya Chama Cha Mapinduzi.
Akinadi sera zake katika kampeni za chama hicho kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dkt. Samia amesema chama hicho kimetekeleza ahadi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa masoko ya kisasa, shule, hospitali na vituo vya afya, pamoja na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja .
Dkt. Samia amesema CCM imeweka mikakati thabiti ya kuongeza ajira kwa vijana, kuimarisha uchumi wa buluu kupitia sekta za uvuvi, mafuta na gesi, pamoja na kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Sauti ya Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amewaomba wananchi kumchagua Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa nafasi ya urais wa Zanzibar, akisisitiza kuwa ndiye kiongozi atakayeendeleza usalama, mshikamano na maendeleo ya Wazanzibari.
Rais Samia amewataka wanachama na wapenzi wa CCM kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi, ili chama hicho kipate ushindi wa kishindo na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.

Sauti ya Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kuendeleza mshikamano na kudumisha amani, akisisitiza kuwa amani ndio msingi wa maendeleo ya nchi.

Sauti ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Naye Mgombea ubunge wa Jimbo la Chaani, Ayoub Mohammed, ameipongeza serikali kwa utekelezaji wa ilani ya CCM kwa zaidi ya asilimia 100, hususan katika sekta ya elimu ya juu kupitia utoaji wa mikopo nafuu na msaada kwa familia zenye changamoto.