Zenj FM
Zenj FM
13 September 2025, 8:41 pm

Na Mary Julius.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuwa endapo atachaguliwa serikali yake itahakikisha inalivuka lengo la kuwaajiri vijana laki tatu na hamsini 350000 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa kampeni za CCM kwa upande wa Zaznibar uliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Zanzibar, Dk. Mwinyi amesema ajira kwa vijana ni miongoni mwa vipaumbele vya serikali yake, na juhudi zaidi zitaelekezwa katika sekta binafsi pamoja na sekta ya umma.
Kuhusu uchumi, Dk. Mwinyi amesema kwa sasa uchumi wa Zanzibar umekua kwa asilimia 7.4, na ana matumaini kwamba ndani ya miaka mitano ijayo utaongezeka hadi kufikia asilimia 10.
Katika juhudi za kukabiliana na changamoto za mfumko wa bei na uhaba wa chakula, Dk. Mwinyi amesema serikali imeazimia kujenga ghala kubwa la kuhifadhi chakula ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha na kuzuia mfumko wa bei
Serikali pia itawekeza zaidi katika ujenzi wa maeneo ya uwekezaji, ili kuvutia wawekezaji na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Balozi Asha-Rose Migiro, Amempongeza Dk. Mwinyi kwa kuendeleza mazuri yaliyofanywa na viongozi waliomtangulia na kuongeza juhudi za maendeleo kwa uaminifu na uwajibikaji mkubwa.
Nae Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Dk. Mwinyi amesimama imara katika kulinda amani na kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa tangu alipoingia madarakani.
AIidha amempongeza kwa kuendeleza sera ya Uchumi wa Buluu, ambayo imeleta fursa nyingi za ajira na miradi ya kimkakati yenye tija kwa wananchi.