Zenj FM
Zenj FM
12 September 2025, 6:18 pm

Na Omar Hassan.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja linamshikilia Mohamed Khamis Hamadi maarufu Edi Mkono(25) Mkazi wa Tunguu Mchamvyani kwa tuhuma za mauaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa PolisI Mkoani Tunguu – Kusini Unguja (SACP) Daniel Shillah amesema tukio hilo lilitokea Septemba 9, 2025 majira ya saa 04:00 usiku huko Tunguu Mchamvyani, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo mtuhumiwa alimshambulia Sheha Hamad Yussuf (29) Mfanyabiashara Mkazi wa Jumbi Mkorogo kwa kumchoma kisu sehemu ya kifuani mwake na kumsababishia kifo.
Kamanda Daniel Shillah amesema kuwa chanzo cha tukio hilo ni mzozo baina ya Marehemu na Mtuhumiwa kufuatia mvutano kwenye biashara ya ndizi, mzozo ambao ulimfanya mtuhumiwa kukasirika na kutoa kisu alichokuwa nacho maungoni mwake na kumchoma marehemu kifuani na kusababisha kifo chake.
Katika tukio jengine Jeshi la Polisi katika Mkoa huo linawashikilia watuhumiwa watatu John Mulembuki (37), Juma Ali Msimu (20) na Mohamed Haji Mussa (18), wote wakaazi wa Kizimkazi Mkunguni kwa tuhuma za wizi wa mafuta aina ya dizeli madumu matano yenye jumla ya lita 100 mali ya kampuni ya CCECC inayojishughulisha na ujenzi wa barabara ya Kizimkazi kupitia Mtende hadi Makunduchi.
Kamanda Shillah ameeleza kuwa watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi na upelelezi ukikamilika mashauri hayo yatafikishwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.