Zenj FM

Magari mapya 25 kuongeza ufanisi wa polisi Zanzibar

11 September 2025, 8:39 pm

Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo akimkabidhi gari Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Elisante Makiko Mmari .

Na Omar Hassan.

Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo amekabidhi magari mapya 25 kwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Vitengo vya Polisi ambazo zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwaajili ya kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi
Akizungumza katika hafla hiyo ya kukabidhi Magari hayo Kilimani, Makao Makuu ya Polisi Zanzibar Kamishna Kombo amemshukuru Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKT. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Kamillus Wambura kwa Jitihada zao za kuimarisha ulinzi na usalama.

Aidha amewataka Makamanda wa mikoa husika kutunza magari hayo na kuzitumia kutoa huduma Bora kwa jamii.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Elisante Makiko Mmari amesema Magari hayo yatapunguza changamoto za usafiri katika kufuatilia, kubaini na kukabiliana na uhalifu.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi Kamisheni ya polisi Zanzibar limepokea magari 11 kwa ajili ya Wakuu wa Polisi Wilaya za Zanzibar.