Zenj FM
Zenj FM
10 September 2025, 9:42 pm

Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar limewakumbusha wananchi wanaotaka kuweka namba au majina binafsi kwenye magari yao kuhakikisha wanazingatia utaratibu uliowekwa kwa kwenda kusajili namba hizo katika Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).
Akizungumza na waandishi wa habari, huko makamo makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar Ziwani, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCP), Naibu Kamishna wa Polisi Zuberi Chembela, amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani (ZARTSA) pamoja na ZRA, limeendesha operesheni ya pamoja ya siku kumi (10) katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Unguja.
Amesema Katika operesheni hiyo, magari yaliyokuwa yamefungwa namba zisizotambulika na mamlaka za usajili kama vile SSH 25-30, MWINYI 2530, TAMBA, na AMEIR URAIS 2025-2023, pamoja na magari yaliyofunga taa za vimulimuli na yale yaliyotumia namba za Tanzania Bara bila kibali, yalikamatwa.
Amesema Jumla ya makosa 2,641 yalibainika katika operesheni hiyo. Kati ya hayo Magari yaliyokamatwa, 814, Pikipiki zilizokamatwa, 1,827 na Jumla ya tozo zilizotozwa ni shilingi milioni mia mbili na thelathini elfu laki sita kumi na nane elfu mia saba na hamsini Tsh 230,618,750/=
Aidha DCP Chembela amesema Jeshi la Polisi linaendelea na Operesheni hiyo na amewataka wananchi kuheshimu sheria za nchi.