Zenj FM
Zenj FM
10 September 2025, 7:29 pm

Ikiwa leo ni siku ya mwisho ya kuwasilisha fomu za kugombea urais kwa upande wa Zanzibar, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imethibitisha kuwa jumla ya vyama 12 kati ya 17 vimerudisha fomu, huku chama kimoja, CUF, kikienguliwa kwa kutotimiza vigezo vya uteuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, amesema mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi CUF, Hamad Masoud Hamad, ameenguliwa baada ya kushindwa kuwasilisha fomu kamili ya wadhamini kutoka mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kwa upande mwingine, mgombea wa urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo Othman Masoud othman amekumbwa na changamoto ya kutokamilika kwa uthibitisho wa uanachama wa baadhi ya wadhamini kutoka mikoa miwili.
Tume imetoa muda wa hadi kesho saa tatu asubuhi kwa ACT-Wazalendo kuthibitisha uanachama wa wadhamini hao.
Akizungumzia maamuzi hayo, mgombea wa CUF, Hamad Masoud Hamad, amesema wameshindwa kuwasilisha fomu ya mkoa wa Kaskazini Unguja kutokana na sababu za kiutendaji ndani ya chama.
Vyama vitano ambayo havijarejesha fomu za kugombea kabisa ni SAU, CCK, UMD, DP, na UPD.