Zenj FM
Zenj FM
8 September 2025, 8:16 pm

Na Mary Julius.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jaji George Joseph Kazi, amewataka waandishi wa habari kuepuka kutumia lugha za chuki, uchochezi, au zinazoleta mgawanyiko wa kijamii kwa misingi ya ukabila, dini, au itikadi.
Akizungumza katika ukumbi wa Tume hiyo Maisara wakati wa mafunzo kwa wadau wa habari kuhusu maandalizi ya uchaguzi, Jaji Kazi amesema ni muhimu kwa waandishi kufuata maadili, kuheshimu haki na kutekeleza wajibu wao kwa weledi wakati wa kuripoti masuala ya uchaguzi.
Aidha jaji kazi amewahakikishia waandishi wa habari kuwa Tume ya Uchaguzi itatoa ushirikiano na mazingira salama ili waandishi wawezekutekeleza majukumu yao kwa uhuru na uadilifu.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Thabit Idarus Faina, amesema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 yanaendelea vizuri, huku akisisitiza wajibu wa wadau wote wa uchaguzi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na usalama.
Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Mpiga Kura na Mawasiliano kwa Umma, Juma S. Sheha, ambaye ametoa mada kuhusu muongozo kwa vyombo vya habari vya umma katika kutangaza kampeni za wagombea, alibainisha kuwa sheria ya uchaguzi inawapa wagombea, mawakala wao na vyama vya siasa haki ya kufanya kampeni kabla ya siku ya uchaguzi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Habari Maelezo, Asha Abdi Makame, amesema waandishi wa habari wana jukumu la kufuatilia na kuripoti kampeni kwa usawa, kwa kuhakikisha kuwa kila mgombea anapata fursa sawa bila upendeleo.
Nao Wadau wa uchaguzi walioshiriki mafunzo hayo wameiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC kushirikiana kwa karibu na Tume ya Utangazaji pamoja na Jeshi la Polisi, ili kuwezesha vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao bila vikwazo au usumbufu.