Zenj FM
Zenj FM
3 September 2025, 7:08 pm

Na Junaina Rajabu.
Jeshi la Polisi mkoa wa Kaskazini Unguja limejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa raia hasa katika kipindi cha kampeni, pamoja na kuimarisha usalama wa barabarani ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.
Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaokiuka sheria za usalama barabarani.
Akizungumza na Zenji FM Radio, Koplo Ali Faki amesema Kikosi cha Usalama Barabarani katika mkoa huo kimeweka mikakati thabiti ya kudhibiti ajali, hasa kipindi hiki cha kampeni, kwa kuwachukulia hatua wote wanaokiuka sheria za usalama.
Kwa upande wake, Sajenti Rukia amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi katika shehia mbalimbali hususan kwa madereva wa bodaboda, ili kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua wakati wa kampeni.
Naye Koplo Ahmada Shida ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa kuhakikisha wanatoa elimu kwa wanachama wao kuhusu umuhimu wa kufuata sheria na kudumisha utulivu wakati wote wa kampeni.