Zenj FM

ZEC yaendelea kutoa fomu kwa wagombea sita wa urais Zanzibar

31 August 2025, 6:22 pm

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George J. Kazi, akimkabidhi fomu ya uteuzi mgombea wa chama cha ACT WAZALENDO ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa ACT na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman.

Na Mary Julius.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George J. Kazi, amekabidhi rasmi fomu za uteuzi kwa wagombea sita wa Kiti cha Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hafla hiyo imefanyika katika Afisi za Tume zilizopo Maisara, Wilaya ya Mjini, Unguja.
Aliye fungua dimba ni mgombea kutoka chama cha NCCR MAGEUZI Laila Rajabu Khamis ambaye amekabidhiwa fomu za kuwania nafasi hiyo na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George Joseph Kazi katika ofisi za Tume hiyo zilizopo Maisara amesema lengo lake kuu ni kuhakikisha vijana wote wenye vyeti maalum wanapata ajira.
Ameahidi kulinda maadili ya Mzanzibari na kuirejesha Zanzibar kwenye misingi ya utu, heshima na maendeleo kama ilivyokuwa enzi za mababu.

Sauti ya Laila Rajabu Khamis.

Naye mgombea wa chama cha ACT WAZALENDO ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa ACT na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, mara baada ya kukabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George Joseph Kazi amesema uzoefu wa muda mrefu katika uongozi na maadili aliyolelewa nayo na wazee wazalendo wa Zanzibar ni chachu ya mabadiliko anayokusudia kuleta.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kumuunga mkono kwa ajili ya kuirejesha Zanzibar mikononi mwa wananchi.

Sauti ya Othman Masoud Othman.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George J. Kazi, ZEC akimkabidhi fomu ya uteuzi mgombea wa chama cha CCK Isha Salim Hamad.

Kwa upande wake mgombea wa chama cha CCK Isha Salim Hamad amesema uamuzi wake wa kugombea ni ushahidi kuwa wanawake wanaweza kuongoza.
Aidha Amesema chama cha CCK kimejiandaa kikamilifu kushinda.

Sauti ya Isha Salim Hamad.

Nae mgombea kutoka chama cha SAU Mwalimu Abdallah amesema amejipanga kuleta ushindani mkubwa kwa vyama vingine.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, ZEC Jaji George J. Kazi, akimkabidhi fomu ya uteuzi mgombea wa chama cha ADA TADEA Juma Ali Khatibu.

Kwa upande wake mgombea wa chama cha ADA TADEA Juma Ali Khatibu Amesema chama chake kina sera ya “Mapinduzi ya Manjano” yenye lengo la kuwaandaa vijana kwa ulimwengu wa utandawazi kupitia elimu ya kiufundi na matumizi ya teknolojia kama vile “alili mremba”.
Aidha amesema ADA TADEA kinamuunga mkono mgombea wa CCM, na kinategemea kupata nafasi ya pili ili kutoa Makamu wa kwanza wa Rais atakaye msaidia Rais wa Zanzibar kuendeleza maendeleo.

Sauti ya Juma Ali Khatibu.

Hatimaye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jaji George J. Kazi, amekabidhi fomu ya uteuzi kwa mgombea UMD Mohamed Omary Shaame ambapo mara baada ya kuchukua fomu ameahidi kuboresha huduma za kijamii kwa kutoa umeme wa unit 100 bure kwa wananchi.
Aidha amesema chama chake kitawajali watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanapewa mishahara kama sehemu ya usawa na haki za kijamii.

Sauti ya Mohamed Omary Shaame.