Zenj FM

Dereva ashikiliwa kwa kusababisha kifo cha mtalii Kusini Unguja

6 August 2025, 8:39 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah.

Na Mary Julius.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja linamshikilia Kassim Omary Ramadhani, mwenye umri wa miaka 30 mkazi wa Fuoni, kwa tuhuma za kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.
Akizungumza na Zenji FM, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah, amesema ajali hiyo imetokea leo katika eneo la Kimbe, Kilima Upepo, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Kamanda Shillah amesema Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili STL 1720, mali ya TRA Zanzibar, ambalo lilikuwa likiendeshwa na Kassim Omary Ramadhani (30), mkazi wa Fuoni dereva huyo alikuwa akitokea Kibuteni kuelekea Makunduchi akiwa amebeba wafanyakazi wenzake wanane.
Amesema alipofika eneo hilo, alijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari, na hivyo kugongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Alphard, lenye namba za usajili Z 913 MH, lililokuwa likiendeshwa na Ussi Khatibu Mapweza (33), mkazi wa Matemwe, ambaye alikuwa amebeba wageni sita raia wa Ubelgiji.
Katika ajali hiyo, mtalii mmoja aliyefahamika kwa jina la Said Mdauchi raia wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 63, alifariki dunia baada ya kupata majeraha makubwa kichwani.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya taratibu zaidi.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah.

Kamanda Shilla ametoa wito kwa madereva wote kuendesha kwa tahadhari na kuwajali watumiaji wengine wa barabara ili kuepusha ajali,

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Shillah,