Zenj FM
Zenj FM
6 August 2025, 4:17 pm

Staf Sajenti Ali Abdalla Juma kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar, amewataka wazazi kuwa makini na watoto wao wanaoendesha vyombo vya moto, kwa kuhakikisha hawapati usukani kabla ya kupata leseni.
Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Zanzibar limewataka wamiliki wote wa vyombo vya moto, ikiwemo magari na pikipiki, kuhakikisha kuwa wanaowaajiri au kuwakabidhi vyombo hivyo wana leseni halali za udereva, ili kusaidia kupunguza ajali za barabarani.
Wito huo umetolewa na Staf Sajenti Ali Abdalla Juma kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Mwangaza wa Habari kilichorushwa na Zenji FM.
Amesema Jeshi la Polisi limejipanga vyema kuimarisha kampeni za kudhibiti ajali kwa kushirikiana na jamii, wamiliki wa magari, wazazi na vyuo vya za udereva.
Sajenti Juma amesema wamiliki wa vyombo vya moto wana mchango mkubwa katika kuzuia ajali kwa kuhakikisha madereva wao wanafuata sheria za usalama barabarani.
Akizungumzia hali ya ajali katika Mkoa wa Mjini Magharibi sajenti juma amesema bado si ya kuridhisha, huku Wilaya ya Magharibi A na B zikitajwa kuwa na idadi kubwa ya ajali ukilinganisha na Wilaya ya Mjini.
Amewasihi abiria kuacha kushabikia mwendo kasi na badala yake wawasimamie madereva ili kuhakikisha wanazingatia sheria zote za usalama barabarani.
Kuhusu mashindano ya CHAN, amewataka madereva kuzingatia njia zilizoruhusiwa na kuendelea kuonyesha uzalendo kwa kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa barabara.