Zenj FM

Polisi, vyombo vya habari watajwa chanzo uchaguzi wa amani

24 July 2025, 1:29 pm

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohammed Ali Ahmed, akizungumza wakati akifunga kongamano la kuimarisha amani kupitia hoja na mijadala ya maelewano kati ya Jeshi la Polisi na vyombo vya habari, lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani Zanzibar.

Na Mary Julius.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohammed Ali Ahmed, amesema amani ni kipaumbele kikuu cha viongozi wakuu wa Tanzania hivyo wadau wote wa uchaguzi wanatakiwa kuhakikisha amani inadumu kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.
Naibu ameyasema hayo wakati akifunga kongamano la kuimarisha amani kupitia hoja na mijadala ya maelewano kati ya Jeshi la Polisi na vyombo vya habari, lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani Zanzibar, amesema maendeleo yanayoonekana nchini Tanzania ni kielelezo tosha cha amani
Mohammed amesema Jeshi la Polisi na wanahabari wana jukumu kubwa la kulinda amani hiyo , kuhimiza maadili, na kusimamia haki na uhuru wa wadau wote wa uchaguzi.
Amesema wanahabari wanapaswa kuelimisha umma na kuepuka kusambaza habari zinazochochea chuki, hasira, na mvurugano, kwani vyombo vya habari vikitumiwa vibaya vinaweza kuwa silaha ya kusababisha machafuko.
Amesema Kongamano hilo limeleta uelewa mpya juu ya umuhimu wa ushirikiano na kujenga mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Jeshi la Polisi na wanahabari, pamoja na kuwa na utaratibu wa kushughulikia migogoro kabla, wakati, na baada ya uchaguzi.
Aidha Amewakumbusha wadau wa uchaguzi kuwa sheria za nchi bado zinaendelea kuwepo na Jeshi la Polisi lina jukumu la kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya yeyote atakayevunja sheria hizo.

Sauti ya Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohammed Ali Ahmed.

Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini DCP David Misime , amewaasa waandishi wa habari kuacha kutoa taarifa za upotoshaji na badala yake watoe taarifa sahihi zenye kuzingatia maadili ya kazi yao.

Sauti ya Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini DCP David Misime.

Mada tano ziliwasilishwa na kujadiliwa katika kongamano hilo ambazo ni muhimu si tu wakati wa uchaguzi bali kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla