Zenj FM

Wenye ulemavu waiomba Tanzania kusaini mkataba wa Afrika ADP

11 July 2025, 4:04 pm

Mkufunzi kutoka Umoja Wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar UWZ, Hababuu Makame akizungumza katika mafunzo maalum yaliyofanyika katika Skuli ya Tumekuja.

Nchi ambazo zimesaini Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu (African Disability Protocol, ADP),ambao umeanza kutumika rasmi tangu Mei 2024 ni Angola, Burundi,Cameroon, Congo Brazzaville, Kenya, Mali, Malawi, Msumbiji, Namibia, Niger, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, Uganda, na Zimbambwe.

Na Mary Julius.

Mratibu wa Kikundi cha Wanawake Wenye Ulemavu Kusini (WUKU), Khairun Khalid Mambo, amesema ipo haja kubwa ya kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu ili wauelewe Mkataba wa Afrika kwa Watu Wenye Ulemavu (African Disability Protocol – ADP) na kuweza kuutetea hadi usainiwe rasmi na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza katika mafunzo maalum yaliyofanyika katika Skuli ya Tumekuja, Khairun amesema ni muhimu watu wenye ulemavu kuwa na maarifa ya kutosha kuhusu haki zao ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa utetezi wa mkataba huo.

Aidha Ametoa wito kwa watu wenye ulemavu kuendelea kujifunza na kujenga hoja madhubuti zitakazowawezesha kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Sauti ya Mratibu wa Kikundi cha Wanawake Wenye Ulemavu Kusini (WUKU), Khairun Khalid Mambo.

Akiwakilisha mada ya usimamizi bora wa fedha , mkufunzi kutoka Umoja Wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar UWZ Hababuu Makame, amesema migogoro mingi inayozikumba taasisi ndogo ndogo za kijamii husababishwa na usimamizi usiofaa wa fedha, hivyo ni muhimu kuwajengea wanavikundi uwezo ili kuepusha changamoto hizo.
Aidha, amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia masomo yote waliyopewa ili vikundi vyao viwe mfano wa kuigwa na hivyo kuwavutia wafadhili kuendelea kuwasaidia.

Sauti ya Mkufunzi kutoka Umoja Wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar UWZ Hababuu Makame.

Kwa upande wao Washiriki wa mafunzo hayo wamesema utekelezaji wa Mkataba wa Afrika kwa Watu Wenye Ulemavu utasaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wanapata haki zao za msingi katika nyanja mbalimbali kama vile elimu, afya, ajira na miundombinu.
Aidha Wamesema kupitia mafunzo hayo, wamepata uelewa wa kutosha wa kujenga hoja za msingi zitakazowasaidia kushawishi Serikali ya Tanzania kusaini na kutekeleza mkataba huo.

Sauti za Washiriki.