Zenj FM
Zenj FM
8 July 2025, 2:47 pm

Na Is-haka Mohammed.
Chama cha Wananchi CUF kimedhamiria kufanya tathmini ya kina ya wagombea watakaosimamishwa katika nafasi mbalimbali za uongozi, kwa lengo la kuhakikisha wanachaguliwa viongozi wenye sifa ya uzalendo na utayari wa kuwatumikia wananchi, si kwa maslahi binafsi.
Akizungumza katika kikao maalum na viongozi na wanachama wa CUF kutoka wilaya nne za Pemba, kilichofanyika katika ukumbi wa Samail Gombani, Chake Chake, Katibu Mkuu wa CUF, Husna Mohd Abdallah, amesema chama hicho kimejipanga kikamilifu katika kuwatetea wananchi na kuwaletea maendeleo endelevu.
Aidha, amesema maamuzi ya uteuzi wa wagombea yatategemea zaidi uzalendo, uwajibikaji na uwezo wa kutatua changamoto za wananchi, huku akihimiza wanachama kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maamuzi ya chama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Wilaya za CUF Pemba, Mbwana Ali Mbwama, amesema tayari zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali limeanza rasmi, na baadhi ya wanachama wameanza kujitokeza kuomba ridhaa ya chama ili kuteuliwa.
Naye Mkurugenzi wa Itifaki na Udhibiti wa CUF, Rajab Mbarouk Mohd, ametoa tahadhari kwa baadhi ya wanachama ambao lengo lao ni kukivuruga chama.
Amesema chama kina utaratibu wa kuwatambua watu wa aina hiyo, na hawatapata nafasi ya kuharibu taswira ya CUF.