Zenj FM
Zenj FM
3 July 2025, 10:54 am

Na Mary Julius.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC, Thabit Idarus Faina, ametangaza kuwa Tume hiyo imewafuta jumla ya wapiga kura 3,352 waliobainika kupoteza sifa za kuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi.
Akizungumza kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Faina amesema kuwa katika utekelezaji wa zoezi la Uendelezaji wa Daftari hilo, Tume iliweka wazi orodha ya wapiga kura waliopoteza sifa kuanzia Mei 24 hadi 30, 2025, ili kutoa fursa kwa wananchi kuweka pingamizi endapo kuna makosa au upungufu wowote.
Baada ya uchambuzi na uthibitisho wa taarifa hizo, Tume kupitia Mkutano wake wa 4 wa mwaka huu uliofanyika Julai 2, 2025, imejiridhisha kuwa wapiga kura waliotajwa hawana tena sifa za kuwemo katika Daftari, na hivyo kuamua kuwaondoa rasmi.
Aidha Mkurugenzi Faina ametoa takwimu za wilaya kwa wale waliopoteza sifa kama ifuatavyo Wilaya ya Micheweni 239, Wilaya ya Wete 325, Wilaya ya Kaskazini A 232, Wilaya ya Kaskazini B 396, Wilaya ya Chake Chake 157, Wilaya ya Mkoani 215, Wilaya ya Kati 355, Wilaya ya Kusini 440, Wilaya ya Magharibi A 221 ,Wilaya ya Magharibi B 285 na Wilaya ya Mjini 487.