Zenj FM

Wanawake wenye ulemavu wahamasishwa kushiriki katika mchakato wa ADP

29 June 2025, 12:29 am

Muwezeshaji kutoka Umoja wa Watu Wenye Ulemavu,UWZ Mohammed  Mohammed

Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanawake kuelewa Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (African Disability Protocol – ADP) na kujifunza mbinu mbalimbali za kuutetea.

Na Mary Julius

 Wanawake wenye ulemavu wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na kujumuika kwenye mijadala mbalimbali ili kuhakikisha wanahusishwa ipasavyo katika mchakato wa kuanzishwa kwa Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (African Disability Protocol – ADP).

Wito huo umetolewa na Mratibu wa kikundi cha Wanawake  Wenye Ulemavu Kusini WUKU Khairun Khalid Mambo katika mafunzo  yaliyo dhaminiwa na  shirika la Action on Disability and Development (ADD), ambayo ni  mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu yaliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Tumekuja, wilaya ya Mjini.

 Khairun amesema  lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanawake kuelewa mkataba huo na kujifunza mbinu mbalimbali za kuutetea.

Amesema ni muhimu wanawake wenye ulemavu kutoa sauti zao, kueleza changamoto wanazokutana nazo, na kushiriki katika kupanga mikakati jumuishi ya utekelezaji wa mkataba huo, unaolenga kulinda haki za watu wenye ulemavu kwa kuzingatia mila na mazingira ya Kiafrika.

Sauti ya Mratibu wa kikundi cha Wanawake  Wenye Ulemavu Kusini WUKU Khairun Khalid Mambo .

Naye, Muwezeshaji kutoka Umoja wa Watu Wenye Ulemavu,UWZ Mohammed  Mohammed amesema  wanawake wengi wenye ulemavu hukumbwa na utegemezi mkubwa na mara nyingi hawana nafasi ya kushawishi au kudai haki zao.

Hivyo, mafunzo hayo yatakuwa kichocheo cha kuwajengea uwezo wa kiakili na kuwapa mbinu za kufanya ushawishi kwa ufanisi.

Sauti ya Muwezeshaji kutoka Umoja wa Watu Wenye Ulemavu,UWZ Mohammed  Mohammed.

Kwa upande wake, Mkufunzi Mary Julius aliyewasilisha mada kuhusu mbinu za kushirikiana na vyombo vya habari katika kutetea haki za watu wenye ulemavu, amewahimiza wanawake hao kutumia vyombo vya habari kueleza mafanikio na changamoto wanazokumbana nazo.

Aidha amesema vyombo vya habari ni nyenzo muhimu ya kuwajengea ujasiri watu wenye ulemavu na kusaidia kupunguza unyanyapaa katika jamii.

Nao Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuhamasika na watahakikisha elimu waliyoipata inawafikia wanawake wengine wenye ulemavu ili wote watambue haki zao na kuzidai kwa njia sahihi.

Sauti ya Washiriki.