Zenj FM

CCM yatilia mkazo ushiriki wa watu wenye ulemavu katika uchaguzi mkuu

12 May 2025, 12:36 pm

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa akizungumza katika kongamano la ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.

Mary Julius.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, ametoa wito kwa watu wenye ulemavu nchini kuacha kuwa watazamaji na badala yake kuwa wahusika wakuu katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa dola mwaka 2025.
Wito huo ameutoa katika kongamano la ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Unguja.
Dkt. Dimwa amesema haki, usawa, na ushiriki wa kundi hilo ni ajenda ya kitaifa inayopewa kipaumbele na CCM.
Dkt. Dimwa amesema kwa mujibu wa Ibara ya 215 ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025, serikali kupitia chama hicho imeweka msingi imara wa kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa vitendo.
aidha Dkt. Dimwa ametumia fursa hiyo kuwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kwa kusimamia vyema miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kufungua fursa za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa watu wenye ulemavu.
Naye Mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi kutoka kundi la watu wenye ulemavu, Mwantatu Mbaraka Khamis, amesema lengo la kongamano hilo ni kuwahamasisha watu wenye ulemavu kutoka makundi yote kushiriki katika uchaguzi na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Mwantatu ,amezipongeza Serikali zote mbili kwa kuendelea kuweka mazingira bora kwa kundi hilo kupata haki na fursa zinazowajengea uwezo wa kijamii na kiuchumi.
Mwakilishi huyo,amesema suala la usawa sio upendeleo, bali ni haki kwa watu wenye ulemavu, mwaka 2025 sio wa kusubiri bali ni wa kushiriki, kuongoza na kuamua hatma ya taifa.
Kongamano hilo lililoandaliwa na mwakilishi Mwantatu Mbaraka Khamis, kwa kushirikiana na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar lilikuwa na mada mbalimbali za kuwajengea uwezo juu ya masuala ya kiuchumi,kijamii na kisiasa.