Zenj FM

Dkt. Khalid atoa wito wadau wa uchukuzi kushiriki mkutano Zanzibar

25 April 2025, 5:13 pm

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohammed.

Na Mary Julius.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohammed ametoa wito kwa wadau wa sekta ya uchukuzi nchini Tanzania, Afrika Mashariki na bara la Afrika kushiriki mkutano wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha kwa kanda ya Afrika na Asia .
Ametoa wito huo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Ofisini kwake Kisauni Dk. Khalid amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kujadili na kutambua fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji zinazotokana na jitihada zinazoendelea za serikali zote mbili ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha miundombinu na kukuza sekta ya usafirishaji na uchukuzi.
Amesema mkutano huo utatoa fursa ya kipekee kwa wadau kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kuanzisha ushirikiano mpya utakaosaidia katika kuimarisha biashara ya kimataifa, kuongeza ufanisi wa huduma za forodha na kuhamasisha maendeleo ya sekta binafsi katika usafirishaji wa bidhaa na huduma.
Aidha waziri amesema mkutano huo umeletwa nchini kwa wakati muafaka kutokana na mafanikio yaliyofanywa na serikali zote mbili katika miradi mbalimbali ya kimkakati katika kurahisisha usafiri , mawasiliana na uchukuzi.

Sauti ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohammed.

Kwa upande wake Rais wa Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio amesema mkutano huo utaweka wazi fursa zilizopo Tanzania kwa jamii ya kimataifa, ili kuvutia wawekezaji na washirika wa biashara.
Aidha Urio, amesema kufanyika kwa mkutano huu Zanzibar ni kutokana na serikali jamuhuri ya muungano wa tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar kuonyesha dhamira ya dhati katika kuhakikisha sekta ya usafirishaji na vifaa (logistics) inakuwa uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.

Sauti ya Rais wa Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio.

Kwa upande wake, Rais wa Mawakala wa Forodha Zanzibar ZFB, Omar Hussein Mussa amesema mkutano huo utatoa jukwaa la kipekee kwa wanachama na washiriki mbalimbali kukutana na kushiriki katika majadiliano, kubadilishana uzoefu na kutengeneza mitandao ya biashara.

Sauti ya Mawakala wa Forodha Zanzibar ZFB, Omar Hussein Mussa.

Mkutano huo utakaofanyika tarehe 30 hadi tarehe 1 may ukiwa na kauli mbiu ushirikiano katika uchumi wa buluu kubadilisha lojistiki na uchumi kwa uendelevu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan .