

7 February 2025, 4:51 pm
Na Omar Hassan
Watendaji wa Madawati ya Jinsia na watoto ya Jeshi la Polisi wametakiwa kuongeza nguvu katika kushughulikia Kesi za Udhalilishaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ili kudhibiti matukio hayo na kuifanya jamii ibaki salama.
Akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa Madawati ya Jinsia na watoto wa Mikoa ya Zanzibar, kwa niaba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mkuu wa Utawala na Rasilimali Watu wa Polisi Kamisheni ya Zanzibar Naibu Kamishna wa Polisi DCP Simon Thomas Chillery amewataka watendaji hao kuyashughulikia kwa haraka na umakini mkubwa matukio ya udhalilishaji ili yafanikiwe Mahakamani.
Nae Mkuu wa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto kutoka Makao Mkuu ya Polisi, Dodoma Naibu Kamishna wa Polisi DCP Maria Nzuki amesema ukatili wa kijinsia na ukatili kwa watoto bado ni tatizo katika jamii za Tanzania hivyo bado kuna haja ya kila mmoja ana wajibu wa kuchukua hatua ili matukio hayo yasitokee.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Tuungane Kuzuia Ukatili wa Kijinsia ili Kuharakisha kufanikisha Malengo ya Uchumi wa Buluu Zanzibar, kutokaShirika la UN Women Lucy Shana amesema Shirika hilo linawakutanisha watendaji wa Madawati ya Jinsia ya Jeshi la Polisi ili kuwa na mikakati ya Pamoja na kuwa na njia bora Zaidi za kufanikisha majukumu ya kuzuwia ukatili.