Zenj FM

Elimu ya matumizi sahihi ya barabara bado inahitajika Zanzibar

20 November 2024, 5:59 pm

Mkuu wa kituo cha umahiri cha kikanda cha usalama barabarani kutoka Dare Es Salam (NIT ) Godlisten Msumanje akizungumza na madereva wa vyombo vya moto, huko Mahonda Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

Na Thuwaiba Mohammed.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Othman Ali Maulid amewataka madereva wa Mkoa wa Kaskazini A Unguja kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani na kufata sheria zilizowekwa na mamlaka husika ili kuepusha ajali zinazoepukika.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Kaskazini A Unguja wakati akifungua mafunzo ya usalama barabarani yaliyotolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar kwa madereva na makondakta wa gari za abiria kutoka Mahonda Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

Amesema elimu zaidi inahitajika kwa jamii na madereva juu ya matumizi sahihi ya barabara.

Aidha Othman Amewataka madereva hao kuzingatia elimu watakayoipata katika mafunzo hayo na kuwa mabalozi wazuri kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani pamoja na kuwalinda watumiaji wengine wa barabara.

Akitoa mada katika mafunzo hayo Mkuu wa Kituo cha Kikanda cha Umahiri katika Usalama Barabarani – NIT, Godlisten Msumanje amesema ili kuondokana na ajali za barabarani ni lazima serikali iongeze juhudi katika kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya barabara kwa makundi mbalimbali wakiwemo madereva, makondakta, madereva wa bodaboda nk.

Aidha amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo madereva na makondakta juu ya matumizi sahihi ya barabara, alama za barabarani, sheria za usalama barabarani ili kujikinga na ajali za barabarani pamoja na kuwalinda watumiaji wengine wa barabara hususani waenda kwa miguu.

Sauti za Enjinia Mhoja Mahona na Mkuu wa Kituo hicho Godlisten Msumanje

Nao baadhi ya waliopatiwa mafunzo hayo wameishukuru NIT kwa kuwapatia mafunzo hayo na kuiomba serikali kushirikiana na NIT kutoa mafunzo hayo mara kwa mara ili kuboresha utendaji wa kazi zao.

Sauti ya baadhi ya waliopatiwa mafunzo.

Mafunzo hayo ya usalama barabarani yameandaliwa na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar kwa kushirikiana na kituo cha Kikanda cha Umahiri katika Usalama Barabarani kutoka (NIT).