Zenj FM

Saba mbaroni kwa kufanya mauaji Mkoa wa Mjini Magharib

3 October 2024, 5:29 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, SACP. Richard Thadei Mchomvu Akizungumza na waandhishi wa habari  huko Madema.

Na Salhey Hamad

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watuhumiwa 05 ambao wamehusika katika matukio mawili ya mauaji yaliyotokea huko Kisakasaka na Mombasa Kwamchina Wilaya ya Magharibi B, pia linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji lililotokea Kijichi Wilaya ya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza na waandhishi wa habari  huko ofisini kwake Madema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib Unguja Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Richard Thadei Mchomvu amesema Mnamo tarehe 06/09/2024 majira ya saa 02:00 asubuhi huko Kisakasaka Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi, mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Kambalagula Mabula Chungwa m/me miaka 45, mnyantuzu wa Fuoni Kibondeni alipatikana akiwa ameshafariki dunia na mwili wake kutelekezwa pembezoni mwa barabara huku mwili huo ukiwa na majeraha yaliyosababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa hiyo lilifanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Wile Dotto Ndombe mwanamke, miaka 28 Mnyamwezi wa Kisakasaka ambae alikamatwa tarehe 15.09.2024 huko Kimanzichana Mkoa wa Pwani na watuhumia wengine wawili walikamatwa Zanzibar.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, SACP. Richard Thadei Mchomvu.

Katika tukio lingine Kamanda Richard amesema, mnamo tarehe 28.09.2024 majira ya saa 08:00 usiku,jeshi la polisi  lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 02 waliohusika na tukio la pili la mauaji ya Idarous Masoud Omar Mme, Miaka 23, Mshirazi Wa Tomondo ambae aliuawa tarehe 20.09.2024 majira ya saa 11:00 alfajiri huko maeneo ya Mombasa Wilaya ya Magharibi B.

Marehemu alituhumiwa kwa kosa la wizi wa pikipiki, ambapo akiwa na wenzake walifanya unyang’anyi wa pikipiki ndipo mmiliki wa pikipiki hiyo alipiga kelele kuomba msaada kwa wananchi.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, SACP. Richard Thadei Mchomvu.

Aidha Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji yaliyofanyika tarehe 24/9/2024 huko Kijichi Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharib ambapo Ramadhan Iddi Shaaban miaka 49 mshirazi wa Kihinani alikutwa amefariki dunia na mwili wake kutelekezwa kwenye pori la Kijichi maarufu Kijichi Spice Farm.

Kamanda Richard amesema Uchunguzi wa awali ulibaini kwamba kifo chake kilitokana na kushambuliwa na vitu vyenye ncha kali na kupelekea majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, SACP. Richard Thadei Mchomvu.

Katika tukio lingine Kamanda Richard amesema mnamo tarehe 02/10/2024 majira ya saa 03:00 usiku huko maeneo ya Kijichi Nguruweni Wilaya ya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Masaka Juma Masaka maarufu Zahoro, miaka 40 mkaazi wa kijichi Nguruweni alimshambulia mkewe Zaituni Elias Kahindi kwa kumpiga mchi kichwani na kupelekea kufariki dunia.

Chanzo cha tukio ni ugomvi miongoni mwa wanandoa hao.

Aidha baada ya tukio hilo mtuhumiwa alitoroka mpaka alipoonekana leo tarehe 03.10.2024 majira ya saa 12:30 asubuhi huko Kijichi akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba aliyofunga kwenye mti wa mfenesi ambapo kifo chake kilitokana na msongo wa mawazo kutokana na kufanya mauaji ya mke wake.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, SACP. Richard Thadei Mchomvu.