Wananchi watakiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi
28 May 2024, 4:30 pm
“Mnaosimamia upelelezi chukueni hatua kesi zipate mafanikio mahakamani” amesema D/DCI Chembera.
Na Omar Hassan / Said Bakar
Viongozi wanaosimamia Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika ngazi ya Mikoa, Wilaya na Vituo vya Polisi wametakiwa kuwasimamia wapelelezi kutimiza wajibu wao na kuwakamata mashahidi wanaoshindwa kufika kutoa ushahidi ili kesi zisishindwe kupata hatia Mahakamani.
Akizungumza na Wakuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mikoa, Wilaya na Vituo, huko Makao Makuu ya Polisi Zanzibar Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi DCP. Zubeir Chembera amesema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya mashahidi kutofika kutoa ushahidi Mahakamani hali inayopelekea kesi kushindwa Mahakamani na Watuhumiwa wa Makosa mbalimbali kuachiwa huru.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Polisi Omar Khamis Abdallah Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kaskazini Unguja amewataka wananchi kuacha muhali na kuepuka kuzimaliza kesi kwa mapatano na badalayake kufika Mahakamani kutoa ushahidi ili lengo la kuekwa adhabu lifikiwe.