ACT wazalendo Zanzibar wajipanga kuelekea uchaguzi mkuu 2025
19 May 2024, 5:51 pm
Na Mary Julius.
Viongozi wa chama cha ACT wazalendo Mkoa wa Kaskazini A na B kichama wametakiwa kuwaorodhesha wanachama wa chama hicho waliopo katika mikoa yao ikiwa ni maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo na Makamu wa Kwanza Wa Rais Othman Masoud amesema sheria ya uchaguzi Zanzibar inapaswa kufanyiwa marekebisho ikiwemo kuondoa utaratibu wa vyombo vya ulinzi na usalama kupiga kura ya mapema kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwaka 2025.
Othman amesema hayo alipokuwa akihutubia mkutano viongozi wa mikoa miwili ya kichama uliofanyika ukumbi wa chuo cha ufundi mkokotoni Mkoa wa kaskazini Unguja.
Aidha amesema kila mwananchi wa Zanzibar anahaki ya kupewa cheti cha kuzaliwa na kitambulisho cha mzanzibari mkaazi pamoja na haki ya kuandikishwa kuwa mpiga kura na kutaka mamlaka zamana kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa huduma hizo.
Naye Makamu Mwenyekiti Wa Chama Hicho Ismail Jussa amesema chama chake kimejipanga kuhakikisha kinaleta mabadiliko ya utawala katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na tayari wameandaa mpango wa kuhakiki wachama na wafuasi nyumba kwa nyumba ili kupata takwimu sahihi za wapiga kura katika chama hicho.
Aidha amesema zama za utawala wa ccm zitafikia ukingoni baada ya uchaguzi mkuu wa 2025 na kuwataka wanachama wa ACT kujenga umoja na mshikamano na kujiepusha na fitina ambazo zinaweza kuvuruga umoja ndani ya chama hicho.
Chama cha ACT Wazalendo kinaendelea na mikutano katika kisiwa cha unguja baada ya kukamilisha ziara kama hiyo kisiwani pemba yenye malengo ya kuwashukuru wanachama baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa viongozi ndani ya chama hicho na kutumia muda mwingi kukosoa vitendo vya rushwa na ufisadi ndani ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.