Viongozi Zanzibar watakiwa kuhamasisha ulinzi shirikishi
29 November 2023, 1:52 pm
Jukumu la usalama wa wananchi si la Jeshi la Polisi pekee hivyo uwepo wa vikundi hivyo utasaidia kupunguza ongezeko la vitendo vya kihalifu katika jamii.
Na Omar Hassan.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad amewataka wananchi kujitolea kujiunga na vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuendeleza amani iliyopo Nchini.
Amesema jukumu la usalama wa Wananchi si la Jeshi la Polisi pekee hivyo uwepo wa vikundi hivyo kutasaidia kupunguza ongezeko la vitendo vya kihalifu katika jamii.
Akizungumza wakati wa akifungua kongamano la ulinzi shirikishi huko Ukumbi wa Skuli ya Dk Ali Muhammed Shein amesema kuwepo kwa Vikundi hivyo kutasaidia kupunguza wahalifu ndani ya jamii.
Aidha amesema kongamano hilo litaisaidia jamii iliyoshiriki kujua lengo la kuanzishwa kwa vikundi vya polisi jamii pamoja na kufanya kampeni ili jamii hiyo iweze kujiunga kusaidia vita dhidi ya vitendo viovu.
Aidha CP Hamad amewataka Wananchi kushirikiana na Jeshi hilo katika kutoa ushahidi wa kesi mbali mbali zinazojitokeza katika jamii sambamba na kuwataka kutoa taarifa mapema za udhalilishaji ili kuweza kupatikana kwa ushahidi.
Nae Mratibu wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma Dk Ezakiel Kyogo amewataka wazazi na walezi kuwapa watoto mafundisho waliyokuwa wakipewa zamani ili kuzuia mporomoko wa maadili katika jamii ya Zanzibar kwa maslahi ya Taifa la kesho.
Nao Baadhi ya washiriki katika Kongamano hilo wamelishukuru jeshi la polisi kwa kuwapaatia elimu juu ya ulinzi shirikishi Sambamba na kulitaka jeshi hilo kuwa na programu maalumu kati ya jeshi la polisi, vikundi vya ulinzi shirikishi na wizara ya Elimu ili waweze kuzibiti vitendo vya uhalifu kati Taifa letu.
Kongamano hilo la siku moja limewashirikisha Wazazi ,walezi, Masheha wa Shehia zaidi ya 50,wanafunzi wa Skuli mbalimbali,Vikundi vya Ulinzi Shirikishi na Maafisa wa Jeshi la Polisi wakijadili umuhimu wa uwepo wa Ulinzi shirikishi katika Jamii.