Fawe yawafikia wajasiriamali Kusini Unguja
8 November 2023, 5:22 pm
Mafunzo hayo ni utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi unaoendeshwa na FAWE ndani ya mkoa wa Kusini Unguja ambapo jumla ya wajasiriamali 723 wamefikiwa kati ya hao wanawake ni 671 na wanaume ni 53.
Na. Ahmed Abdulla.
Wajasiriamali kutoka vijiji vya Kajengwa na Paje wamesema kupatiwa kwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutambua mbinu na fursa za kupata mikopo inayotolewa na serikali yamewaamsha na kuanza mchakato wa ufuatiliaji wa mikopo hiyo ili kufikia lengo la kujikwamua na umasikini.
Wameyasema hayo huko katika skuli ya maandalizi Kajengwa na skuli ya maandalizi Paje mara baada ya kupatiwa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Shirika la Kuwawezesha Wanawake Kielimu na Kiuchumi Zanzibar (FAWE) ambapo wamesema kwa sasa ni wakati sahihi kwao kwenda kwenye taasisi zinazoshughulika ili kuomba mikopo hiyo.
Wamesema mbali na kuomba mikopo hiyo lakini pia wataongeza juhudi katika kufanya shughuli zao mbalimbali za ujasiriamali ikiwemo kilimo cha mwani pamoja na uchakataji wa zao hilo jambo litakaloongeza wingi wa bidhaa zao wanazozipeleka sokoni.
Kwa upande wake Afisa Ufuatiliaji kutoka katika shirika la FAWE, Hasina Suleiman Rashid amesema kumalizika kwa mafunzo hayo ya awamu ya kwanza katika shehia tano za mkoa wa Kusini Unguja FAWE inajiandaa kuwawezesha wajasiriamali kulitumia zao la mwani kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii kutoka wilaya ya Kusini Zakaria Fabian Tinde amesema wilaya ya Kusini itaendelea kuwahamasisha wajasiriamali kuitumia mikopo hiyo kwa ajili ya kuongeza mitaji yao.