Jumuiya ya Serikali za Mitaa Zanzibar yapata viongozi
1 October 2023, 6:56 pm
Na Mary Julius
Kaimu katibu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania ALAT Muhammed Ahmed Maje amesema utekelezaji wa maendelo katika nchi hufanywa kwa kuanzia katika mamlaka za serikali za mitaa.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa uchaguzi wa jumuiya ya serikali za mitaa zanzibar uliofanyika katika ukumbi wa baraza la jiji zanzibar,Kaimu Katibu huyo amesema mamlaka za serikali za mitaa zikifaya vizuri itarahisisha shughuli za maendeleo kwa wananchi.
Aidha amewasihi viongozi watakao changuliwa kuiendeleza jumuiya hiyo kwa kujifunza, na kufanya vikao vitakavyowezesha kujadiliana changamoto na mafanikio pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuepusha migogoro ambayo huchelewesha shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Zainab Khamis Kibwana amesema viongozi watakao chaguliwa watawakilisha jumuiya hiyo katika shughuli zote zitakazo hitaji uwakilishi wa serikali za mitaa kwa upande wa Zanzibar.
Aidha Zainabu amesema lengo la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kudumisha na kukuza maendeleo ya serikali za mitaa pamoja na kutetea haki na maslahi ya serikali za mitaa na kuziwakilisha serikali za mitaa katika kutoa maoni.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Zanzibar ZALGA ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Mahmoud Muhammed Mussa amesema chombo hicho kitatumika kupandisha hadhi ya madiwani na kuhakikisha heshima ya madiwani inaonekana katika jamii na tasisi na kuahidi kuitumikia nafasi hiyo ili kufikia malengo walio jiwekea.