Waandishi wa habari Zanzibar wajengewa uelewa kamisheni ya ardhi
24 September 2023, 4:37 pm
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar Rahma Kassim Ali Amesema wizara hiyo inakabiliwa na changamoto ya migogoro ya ardhi licha ya kuwa na sheria nyingi za ardhi.
Na Mary Julius.
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali amewataka waandishi wa habari kutumia taaluma zao katika kuzielezea sheria za ardhi ili kuzuia migogoro ya ardhi inayo tokana na uwelewa mdogo wa sheria hizo kwa wananchi.
Akizungumza katika semina ya siku moja ya kuwajengea uwelewa waandishi wa habari ili kusaidia kutoa elimu kwa wananchi juu ya kamisheni ya ardhi iliyofanyika katika ukumbi wa wizara hiyo wilaya ya mjini unguja.
Amesema changamoto hizo nyingi zinachangiwa na uelewa mdogo wa wananchi, madalali na hata utoaji wa vibali vya ujenzi kuanzia ngazi ya shehia hivyo kusababisha hata maneo yaliyotengwa kama hifadhi na kilimo kuvamiwa.
Aidha amesema waandishi wa habari ndio sauti ya jamii hivyo ni muhimu kupewa elimu ambayo itasaidia kuwawezesha wananchi kufahamu kupitia vyombo vyao.
Naye Katibu Mtendaji wa kamisheni ya Ardhi Zanzibar, Khamis Juma Khamis, amesema semina hiyo imelenga kutoa taaluma kwa vyombo vya habari ili kushirikiana pamoja katika kuelimisha jamii juu ya shughuli zinazofanywa na Kamisheni hiyo.
Aidha amesema wizara kupitia kamisheni ya ardhi inatarajia kuzindua kampeni ya uhaulishaji wa ardhi Oktoba mwaka huu katika maeneo yote ya Unguja na Pemba na kuanza katika wilaya ya Magharibi B.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mzee Ali Haji, amewataka wananchi wanapotaka kununua ardhi kufika kamisheni ili kutambua eneo wanalonunua lipo salama, kwani yapo maeneo ambayo yamepangwa kwa ajili ya uwekezaji, ujenzi wa miradi na maeneo ya akiba.