Vijana Pemba waomba ajira ujenzi uwanja wa ndege
24 September 2023, 3:08 pm
Wananchi waliopisha ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba kuanza kulipwa fidia mara baada ya kukamilika kwa tathmini.
Na Is-haka Mohammed
Kamati ya muda ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoratibu masuala ya ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba imekutana na wananchi wa vijiji vya Furaha, Mvumoni na Mfikiwa ambao watahamishwa kwenye maeneo hayo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa kujadiliana juu ya malipo ya fidia yanayotegemewa kufanyika hivi karibuni.
Akizungumza na wananchi hao Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri hao ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dkt. Khalid Salim Moh`d amesema tayari ripoti ya mthamini kuu imeshakamilishwa na kukabidhiwa wizara hiyo na hivi punde itakabidhiwa kwa wizara ya fedha ni shughuli za ulipaji zianze.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dkt. Saada Mkuya Salim amewahakikishiwa wananchi hao kuwa fedha kwa ajili ya fidia kwa wananchi hao zipo kilichokuwa kikisubiriwa na ripoti ya mtathmini na muda wowote zoezi la ulipaji litaanza kufanyika.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud amewapongeza wananchi hao kwa uvumilivu mkubwa waliouonyesha kwa serikali na kuwataka kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kifupi kilichosalia.
Kwa upande wao wananchi wa maeneo hayo ambayo ni Furaha, Mvumoni na Mfikiwa wameomba wakati wa utekelezaji wa mradi vijana wao wasiachwe watakapohitaji wafanyakazi wakati wa ujenzi.