Wafanyabiashara Pemba walalamikia kodi kubwa
22 September 2023, 5:01 pm
Wafanyabiashara kisiwani Pemba wameiomba serikali kuwapunguzia kodi ili kuweza kunusuru biashara zao.
Na Is-haka Mohammed.
Wafanyabiashara kisiwani Pemba wamedai kuwepo kwa kodi kubwa kunatishia uhai wa biashara zao na kuiomba serikali kuangalia upya hali ya kodi wanazotoza ili kunusuru hali hiyo isitokee.
Wafanyabiashara hao wameyasema hayo huko Chake Chake Pemba wakati wakizungumzia ugumu wa biashara zao unaosabishwa na kodi wanazotozwa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) pamoja na taasisi zingine za serikali.
Wakizungumzia hali hiyo mfanyabiashara Rashid Nassor Moh`d (Manyimbo) na mwenzake Waziri Salim Waziri wamesema hawakatai kulipa kodi lakini wamekuwa wakishindwa kufuatia hali ngumu ya biashara na kuwepo kwa kodi isiyo rafiki kwao.
Naye Mkurugenzi wa ZRA Pemba Jamal Hassan Jamani amesema kodi ambazo wamekuwa wakitozwa wafanyabiashara hao ni makusanyo kutoka kwa wananachi ambao ndio wanaolipa kodi hizo na pia ameeleza kuwa kodi zinazotozwa zimegawiwa kwa mujibu wa hali za biashara husika.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka wa Mapato Zanzibar ZRA Profesa Hamed Rashid Ikmany aliwataka wafanyakazi wa ZRA kuhakikisha lengo la ukusanyaji wa mapato waliloekewa linafikiwa na kutumia busara katika kutekeleza majukumu yao