Jeshi la Polisi Zanzibar kubadilika kiutendaji
21 September 2023, 7:48 pm
Mafunzo ya mara kwa mara yanayotolewa kwa askari kuhusu haki za binadamu yataweza kuleta mabadiliko ya kiutendaji kwa Jeshi la Polisi Zanzibar.
Na Omary Hassan
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP. Hamad Khamis Hamad amesema Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar linatarajia mabadiliko ya kiutendaji unaozingatia utoaji wa haki kwa wananchi kufuatia mafunzo ya mara kwa mara yanayotolewa kwa askari kuhusiana na haki za binaadamu.
Akizungumza katika mafunzo ya haki za binadamu kwa askari wa polisi mikoa ya Kaskazini na Kusini Pemba huko Madungu wilaya ya Chake chake kisiwani Pemba, amesema ili haki zipatikane kwa wadau wote wa haki hawana budi kubadilika katika utendaji kwa kuzingatia utoaji wa haki.
Naye jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar Jaji Mshibe Bakar amehimiza kutoa kuchukuliwa hatua kwa makosa madogomadogo ya uvunjifu wa haki za binadamu kwani kupuuzwa kwa makosa hayo kunaweza kukasababisha madhara makubwa hapo baadaye.
Kwa upande wake Mkurugezi wa Taasisi ya kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar (ZAFAYCO) Abdalla Abeid amesema jumuia hiyo imejikita kutoa mafunzo ya haki za binadamu kwa askari wa jeshi hilo ili kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria na taratibu na hatimaye kuepusha malalamiko ya jamii dhidi ya jeshi la polisi.