Wizara ya Afya Zanzibar yasambaza vifaa katika hospitali mpya za wilaya
29 August 2023, 2:32 pm
Lengo la kujengwa hospitali za wilaya ni kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuwapunguzia masafa wananchi.
Wizara ya Afya Zanzibar imesema kuanza kutumika hospitali za wilaya zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh ameyasema hayo katika ziara maalum ya kukagua uwekaji wa vifaa katika hospitali za wilaya zinazotarajiwa kuanza kazi mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka huu.
Aidha amesema katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa hospitali hizo suala la uendeshaji na usafi limezingatiwa kwa kupewa kampuni maalum zitakazoendesha na kusimamia hospitali hizo.
Amezitaja hospitali ambazo zitakazoanza kutumika kwa awamu ya Septemba kuwa ni Hospitali ya Wilaya ya Magogoni, Chumbuni, Kivunge kwa upande wa Unguja na Micheweni pamoja na Vitongozi kwa upande wa Pemba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Tiba wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Msafiri Marijani amesema hospitali hizo zitatoa huduma mbali mbali zikiwemo za mama na mtoto, wagonjwa mahututi, dharura na ajali pamoja na upasuaji na kuwataka wananchi kuzitumia hospitali hizo.
Nae Mkuu wa wilaya wa kaskazini ‘A’ Sadifa Juma Khamis ameipongeza wizara ya Afya Zanzibar kwa kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo sambamba na kuwataka wananchi kuzitumia vyema neema hizo.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Kampuni ya Saife Hospitali Dkt. Hamid Farid amesema watahakikisha suala la usimamizi wanalitekeleza vyema ili kuweza kutoa huduma zenye ubora hapa nchini.