Wazazi watakiwa kuwapeleka watoto hospitali kupatiwa huduma ya tohara
29 August 2023, 1:56 pm
Wananchi wametakiwa kutumia fursa ya kwenda kufanya matibabu kwenye kambi inayoendelea katika Hospitali ya Kivunge.
Na Omary Abdallah.
Wizara ya Afya Zanzibar imesema kufanyika kwa kambi za magonjwa mbalimbali hapa nchini kunasadia kwa kiasi kikubwa kuwapatia huduma wananchi kwa ukaribu pamoja na kuweza kupunguza gharama za matibabu.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui ameyasema hayo wakati alipofanya ziara maalumu ya kukagua kambi ya matibabu inayoendeshwa na taasisi ya Peleks kwa kushirikina na Wizara ya Afya na Hospitali ya Kivunge.
Amesema katika kambi inayoendelea katika Hospitali ya Kivunge ambayo inatoa matibabu ya magonjwa mbali mbali yakiwemo magonjwa ya njia ya mkojo Mawe katika figo na magonjwa mengine na tayari wamewafanyia upasuaji watu Zaidi ya 60 wakiwemo watoto kwa magonjwa ambayo yalihitaji ujuzi zaidi na vifaa vya kisasa.
Amesema katika kambi hiyo madaktari hao wameweza kubaini watoto ambao wametahiriwa vibaya na kuwa na tundu zaidi ya moja katika sehemu zao za siri na madaktari hao wameweza kuwafanyia upasuaji na kurudi hali zao kama kawaida.
Kwa upande wake mtaalamu wa Ganzi na Usingizi kutoka Wizara ya Afya Omar Atiki Suleiman ambae anafanya kazi na Tasisi ya Peleks amesema wameweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutoa huduma hospitalini hapo Amefahamisha kuwa lengo ni kuwafanyia upasuaji watu wenye matatatizo ya njia ya mkojo wapatao 200 na watafanya huduma hiyo kwa muda wa siku sita na kuwataka wananchi wenye matatizo ya njia ya mkojo wafike kupata huduma hiyo inayotolewa bila ya malipo.
Kwa upande wa daktari dhamna wa Hospitali ya Kivunge Haji Machano amesema huduma hiyo itakayoendeshwa mpaka tarehe mosi mwezi wa tisa amewataka wananchi wenye matatizo ya njia ya mkojo wakiwemo watoto, watu wazima wanawake na wanaume wenye matatizo hayo kudhurua kupata matibabu.
Amesema huduma inayotolewa katika hospitali ya Kivunge katika kambi hiyo inatolewa na madaktari wabobezi wa nchini Uengereza na kuwataka kutumia fursa hiyo.