Kijana ajinyonga Pemba
27 August 2023, 3:21 pm
Na Is-haka Mohammed
Mtu mmoja anayejulikana kwa jina Moh’d Omar Juma maarufu Magodoro anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 mkaazi wa Machomanne Kilimo amefariki dunia baada ya kuonekana akining’inia katika chumba kwa kujinyonga.
Khamis Issa Moh`d ni Mwanafamilia wa marehemu amesema kijana wao huyo aliingia na kujifungia ndani ya chumba siku ya Ijumaa majira saa nne za asubuhi lakini hakutoka na ndipo ndugu zake walipomgongea usiku lakini hakufungua mlango na walimwacha kwani kwa siku za hivi karibuni ilionekana hiyo kuwa ni kawaida yake.
Amesema ilipofika asubuhi ya Jumamosi na kuona bado hajafungua ndipo walipoamua kuuvunja mlango na kumuona ameshafariki kwa kujinyonga akitumia kanga aliyoifungwa juu ya feni.
Naye ndugu wa marehemu Moh`d, ambaye ni Nassor Omar Juma amesema kaka yake kwa masiku ya hivi karibuni alikuwa ni mgonjwa wa wasiwasi ambapo walifanya juhudi za kupelekea hadi katika hospitali ya afya ya akili Kidongo Chekundu Unguja na baada ya kuonekana hana tatizo katika afya ya akili walirudi naye na kuendelea kuishi nae kwa ukaribu.
Akizungumzia tukio hilo Sheha wa Shehia ya Wara Massoud Moh’d amesema alipokea taarifa za kujinyonga marehemu Moh`d alipofuatwa na ndugu yake akiwa nyumbani kwake kwa ajili ya kutoa taarifa na yeye alichukua hatua ya kutoa taarifa katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Marehemumu Moh`d aliwahi kuwa na mke ambaye waliachana na alibahatika kuzaa naye watoto watatu na tayari mwili wake umeshahifadhiwa katika makaburi ya kijijini kwao Dutani.