ZRA yajisogeza karibu ya walipa kodi Pemba
11 August 2023, 3:21 pm
Na Is-haka Mohammed Pemba.
Katika kuhakikisha wananchi kisiwani Pemba wanalipa kodi kwa ukamilifu Mamlaka ya Mapato Zanzibar imetoa mafunzo kwa walipa kodi Pemba ili kuwajengea uelewa wa mfumo mpya wa kulipa kodi.
Mamlaka ya Mapato Zanzibar ZRA imesema mabadiliko ya mfumo wa ulipaji kodi kwa walipa kodi kutoka ZETRAS kwenda ZITRAS umelenga kurahisisha mawasiliano kati ya ZRA na mlipa kodi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar Jamal Hassan Jamal huko katika ofisi za ZRA Gombani Chake Chake Pemba wakati akifungua mafunzo ya siku tatu juu ya mfumo huo mpya kwa walipa kodi wenye mahoteli kisiwani Pemba.
Amesema mfumo utamwezesha moja kwa moja mlipa kodi kufanya wamasiliasho wa marejesho yake akiwa katika eneo lake la kibiashara na kuondosha usumbufu uliokuwa ukijitokeza kwa wawekezaji.
Kwa upande wake Meneja Huduma za Tehama kutoka Makao Makuu ya ZRA Zanzibar Issac Moh`d amesema mfumo huo wa kisasa utaboresha huduma kwa mlipa kodi.
Nao baadhi ya walipa kodi wanaoshiriki kwenye mafunzo hayo wameipongeza ZRA kwa kuanzisha mfumo huo mpya ambao utawasaidia kupunguza muda na gharama za kupeleka marejesho ofisi za zra Gombani.