Keifo FM

Kyela: CHADEMA stop msaada wa kukarabati barabara Masebe

7 May 2024, 19:20

Pichani ni gari likimwaga mawe yaliyotolewa na CHADEMA wilaya ya Kyela ikiwa ni msaada wa kurejesha hali ya usawa wa barabara ya Masebe Mwaya

CHADEMA wilaya ya Kyela kimezuiwa kuendelea kutoa msaada wa kukarabati barabara ya kijiji cha Masebe iliyoharibiwa na mafuriko hapa wilayani Kyela.

Na James Mwakyembe

Siku chache baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kuanza kutekeleza ahadi ya kumwaga tripu nane za mawe na kifusi katika barabara ya Masebe iliyoharibiwa na mafuriko, serikali ya kata ya Mwaya imepiga marufuku zoezi hilo kuendelea kutekelezwa.

Haya yanajiri ikiwa ni siku chache tu baada ya mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kyela Victoria Swebe kuungana na wadau wengine katika kuitatua kadhia hiyo ya uharibifu wa miundombinu ya barabara ya kijiji hicho ambayo imeachwa baada ya mafuriko.

Akizungumza mbele ya vyombo vya habari akiwa kijijini hapo Swebe amesema amepokea taarifa za kusimamisha utekelezaji kutoka kwa afisa mtendaji wa kijiji cha Masebe ambaye pia amepokea maagizo kutoka kwa afisa mtendaji wa kata ya Mwaya akiagizwa kumsimamisha mdau huyo huku akikiri kuwa sababu hazikuwekwa wazi kwanini zoezi hilo lisitishwe.

Sauti ya mwenyekiti wa CHADEMA Victoria Swebe akizungumza kuhusu marufuku iliyotolewa na serikali

Ameongeza kuwa kutokana na taarifa hiyo wao CHADEMA wamekubali kusitisha jambo hilo huku akieleza kuwa atahakikisha anawasiliana na  viongozi wa serikali ngazi ya wilaya akiwemo mkuu wa wilaya ya Kyela pamoja na mkurugenzi ili kujiridhisha kama taarifa hizo ziko sawa na kisha kuona namna ambavyo chama hicho kitafanya katika kutekeleza msaada huo kwa kuwa waliamua kwa hiari yao kuupeleka kwa wanamasebe.

Sauti ya Victoria Swebe akizungumza kuhusu kukubali kusitisha msaada huo
Pichani Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya Kyela Victoria Swebe akiwa katika eneo la tukio mahali ambapo barabara imeharibiwa akiwa na baadhi ya wajumbe wa chama hicho ikiwemo Ngamanya Mwakasula

Wakizungumzia suala hilo, baadhi ya wananchi wa kijiji cha Masebe wameiomba serikali kupitia mamlaka husika kuliondoa zuio hilo kwani barabara hiyo kuendelea kuwa hivyo ilivyo sasa ni kitendawili kwao kwani usalama wa afya unakuwa rehani kwani hivi karibuni mwanamke mmoja alilazimika kujifungulia katika chumba cha darasa baada ya usafiri kukosa njia

Sauti ya wananchi Masebe wakiomba serikali kuwaruhusu CHADEMA kukakarabari barabara hiyo ili waondokane na kadhia hiyo

Akizungumza kwa njia ya simu mhandisi wa TARURA wilaya ya Kyela Musa Mfungata amekiri kuwepo kwa jambo hilo huku akibainisha kuwa ili jambo kama hilo lifanyike inabidi zifuatwe taratibu za kisheria ikiwemo kuwasilisha taarifa za misaada kama hiyo ili TARURA watoe watalaam watakaosaidia kutoa ushauri wa namna ya kurekebisha barabara.

Sauti ya Mfungata akizungumza baada ya taarifa hiyo kumfikia na hatua zilichokuliwa
Pichani ni Mhandisi wa wilaya ya Kyela Mhandisi Mfungata

Hivi karibuni wilaya ya Kyela imekumbwa na mafuriko sehemu mbalimbali ambapo Masebe ni miongoni mwa maeneo hayo ambayo yameacha kilio kikubwa kwa wananchi wa kijiji hicho kilichopo Mwaya.