Kyela:Madaktari na wauguzi wazembe sasa kukiona chamoto
30 April 2024, 14:10
Katika kuhakikisha kwamba huduma bora za afya zinapatikana katika zahanati,vituo vya afya na hospitali ya wilaya ya kyela serikali imekusudia kuwaondoa kazini watumishi wote walio na lugha mbaya ya matusi kwa wagonjwa hapa wilayani Kyela.
Na James Mwakyembe
Ziara ya mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela kutembelea zahanati zote ndani ya wilaya imehitimishwa rasmi katika hospitali ya wilaya Kyela huku onyo kali likitolewa kwa watumishi wazembe kuwa serikali haitawavumilia kuichafua wilaya.
Ziara hiyo imefanywa rasmi ikiwa na malengo mawili ambayo ni kutazama mapato ya zahanati ndani ya halmashauri pamoja na kutazama mambo mbalimbali ya kiutendaji baada ya kuwepo kwa taarifa kutoka katika baadhi ya zahanati kutokusanya fedha pamoja na kuzitumia nje na matumizi ya serikali.
Akizungumza wakati wa kukamilisha ziara hiyo akiwa katika hospitali ya wilaya ya Kyela Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela Katule Godfrey Kingamkono amepongeza uongozi wa hospitali ya wilaya ya Kyela kukusanya mapato vizuri ambapo hospitali hiyo imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi milioni mia sita na nane kutoka katika makadilio ya bajeti yao ya shilingi milioni miasaba na hamsini.
Pamoja na pongezi hizo alizozitoa kwa uongozi Katule ameongeza kuwa baraza la madiwa lilimwagiza mkurugenzi mtendaji kupitia idara ya afya kuhusu mifumo ya ukusanyaji mapato ambapo lilitolewa agizo la kuwaondoa mawakala waliopo sasa na kazi hiyo kufanywa na hospitali yenyewe.
Katika hatua nyingine Katule amesema ili kuhakikisha mapato hayo yanakusanywa vizuri ni lazma kuboreshwe huduma za afya kwa ngazi ya zahanati,vituo vya afya hadi hospitalini ya wilaya ya Kyela ili kufanya watu wajivunie huduma zinazotolewa na serikali kisha kutoa kalipio kwa wauguzi wanaokiuka taaluma yao.
Katika kuunga mkono uboreshwaji wa huduma za afya hospitalini hapo Kingamkono ametoa televisheni moja kubwa itakayofungwa eneo la kupumzikia watu walio na wagonjwa hospitalini hapo katika eneo lililojengwa upya baada ya lile la kwanza kuendolewa kupisha ujenzi wa barabara ya Ibanda- Itungi Port.
Katule Godfrey Kingamkono ni diwani wa kata ya Ikimba hapa wilayani Kyela ambaye mwaka 2020 alichaguliwa na madiwani wenzake kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya kyela ambapo mpaka sasa ameendelea kushikiria nafasi hiyo kwa kuwatumikia wananchi kuzitatua kadhia mbalimbali zinazowakumba katika maeneo yao.