Luoga: Watanzania niokoeni saratani ya koo inaniua
14 March 2024, 18:12
Dastani Luoga mkazi wa kitongoji cha Roma hapa wilayani Kyela ameomba watanzania kumsaidia michango ya kifedha ili kufanikisha upasuaji wa saratani ya koo inayomsumbua sasa.
Na Masoud Maulid
Baada ya kushindwa kula wala kunywa chochote kwa muda wa miezi minne, sasa Dastani Luoga mkazi wa kitongoji cha Roma wilayani Kyela anaomba msaada kwa watanzania kumsaidia ili aweze kutibiwa tatizo la uvimbe kwenye koo lake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Luoga amesema tatizo hilo limeanza mwaka 2023 mwezi wa Desemba ambapo wakati anakula chakula kilishindwa kupita kwenye koo hali ambayo ilimpa wasiwasi na kwenda hospitali binafsi kwa ajili ya kupata matibabu.
Luoga ameongeza kuwa baada ya kupata ushauri kwenda hospitali ambayo ina vipimo vya koo, alikwenda jijini Mbeya ambapo alifanikiwa kufanyiwa vipimo na kubainika kuwepo uvimbe kwenye koo japo haikufahamika ndani ya uvimbe huo kuna kitu gani hali iliyopelekea kuchukuliwa vipande vya nyama kwenye koo na kupelekwa hospitali ya Rufaa jijini Mbeya kwa uchunguzi zaidi.
Baada ya vipimo ilibainika kuwa ana tatizo la saratani ya koo ambayo ilitakiwa kutoa kaisi cha shilingi milioni mbili na laki tano ili afanyiwe upasuaji jambo ambalo limekuwa gumu kutokana na ukosefu wa fedha hivyo akilazimika kurudi nyumbani kwa ajili ya kutafuta fedha.
Amesema katika kuhangaika kwa namna ya kupata angalau uwezekano wa kuanza hata kula chakula alilazimika kwenda hosptali ya Ikonda iliyopo wilaya ya Makete mkoa wa Njombe ili kupata matibabu zaidi ambapo baada ya kufanyiwa vipimo pia iligundulika saratani ya koo na kushauriwa kwenda hospitali ya Ocean Road ya Dar es Salaam ama KCMC iliyopo Moshi mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa sasa Dastani Luoga anaishi kwa msaada wa mpira ambao umewekwa sehemu ya tumbo lake ambapo chakula chochote laini pamoja na maji vinapitishwa kwenye mpira huo hadi tumboni hivyo anaomba watanzania kumsaidia kwa kiasi chochote kitakachomsadia kupata matibabu kwenye hosptali zilizotajwa kuwa na uwezo wa kutibu tatizo hilo.
Kwa mtanzania au msamaria mwema yeyote anayeguswa na tatizo lake anaweza kuwasiliana na mgonjwa mwenyewe kwa kutumia simu nambari 0656963546 au kuwasilina na meneja wa Keifo FM kwa simu namba 0768767179.